Home Geita Gold FC IKIWA NDIO MARA YAO YA KWANZA…GEITA GOLD WAPEWA RAMANI YA KUTIKISA MICHUANO...

IKIWA NDIO MARA YAO YA KWANZA…GEITA GOLD WAPEWA RAMANI YA KUTIKISA MICHUANO YA CAF MSIMU UJAO…


Geita Gold inaendelea kujiandaa na kukamilisha usajili kwa ajili ya msimu mpya wa mashindano wa 2022/2023 na uongozi wa chama cha soka mkoani Geita (Gerefa) umeibuka na kutia neno juu ya maandalizi hayo.

Geita Gold itashiriki michuano ya Shirikisho barani Afrika, Ligi Kuu Bara na shirikisho la Azam (ASFC) na imeendelea kuimarisha kikosi chake kwa kufanya usajili wa wachezaji wa ndani na nje huku ikitarajia kuweka kambi nchini Burundi.

Mwenyekiti wa Gerefa, Salum Kulunge alisema mipango na maandalizi yanayosukwa na timu hiyo italeta kishindo kikubwa msimu ujao huku akiwatoa wasiwasi mashabiki kuwa timu hiyo haitakata pumzi baada ya kile ilichokifanya msimu uliopita kwani mambo ndiyo kwanza yameanza na kuna makubwa yanakuja.

Alisema baada ya kufanikiwa kukamata nafasi ya nne kwenye Ligi na kukata tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa vigogo wa timu hiyo, wadhamini wake na chama cha soka mkoani humo wanaendelea kuweka mikakati madhubuti itakayowalipa tena msimu ujao na kuifanya timu yao kuwa na mwendelezo mzuri.

“Tunaipongeza timu yetu kwa walichokifanya msimu wao wa kwanza ni mafanikio makubwa tumefuzu kimataifa na kutoa mfungaji bora siyo jambo dogo ni heshima, natoa pongezi nyingi kwao kwa sababu labda wangetupuuza na ushauri wetu lakini wanatusikiliza na wamefanikisha haya.”

“Watu wanakuwa na hofu timu imekuwa na nguvu ya soda kama baadhi ya timu zilivyokuwa lakini klabu hii imejizatiti na imejifunza kupitia wengine waliofanikiwa na kukwama naamini kuna mipango mizuri kati ya timu, wadhamini wake na chama cha soka ili kuwe na mwendelezo bora,” alisema.

Alisema maongezi kati ya chama cha soka, uongozi wa klabu na wadhamini na wadau mbalimbali mkoani humo ya kuiimarisha timu hiyo yanakwenda vyema huku akiwataka wana Geita kushikamana kama ilivyokuwa msimu uliopita ili kikosi kiwe mshindani mkuu na kufanya vizuri zaidi ya msimu ulioisha.

“Ukweli Ligi yetu imekuwa na chachu kubwa kutokana na udhamini uliowekwa timu zinashindana, kwa upande wa timu yetu chachu imekuwa kubwa zaidi imenogeshwa sana na wadhamini wake ambao wameisaidia sana kuwekeza na kuhakikisha wachezaji wanapata stahiki kwa wakati,” alisema.

SOMA NA HII  SABABU ZA SIMBA KUACHANA NA KIPA WAO MBRAZILI ZAWEKWA WAZI