ABDI Hamid Moallin,Kocha Mkuu wa Klabu ya Azam FC ameweka wazi kuwa kunahatihati ya mchezo wao wa kirafiki dhidi ya Simba kutochezwa kulingana na ratiba kuwabana.
Azam FC imeweka kambi nchini Misri sawa na Simba ambazo zote ni za Tanzania ikiwa ni kwa ajili ya maandalizi ya msimu wa 2022/23.
Moallin amesema kuwa mpango mkubwa upo kwenye kucheza mechi za kirafiki na miongoni mwa timu ambayo alikuwa anahitaji kucheza nayo ni pamoja na Simba.
“Tulikuwa na mpango wa kucheza na Simba ila kwa bahati mbaya wao watarudi mapema sisi tukiwa kwenye ratiba ya kucheza mechi ya pili hivyo itakuwa ni bahati mbaya kwetu kama itafanikiwa itakuwa vizuri lakini mazingira yanaonesha haitawezekana.
“Tutacheza kwanza na Wadi Degla kisha tutacheza na Suez zote hizi ni timu nzuri na kuna uwezekano tukapata mchezo wa tatu kabla ya kurudi Dar es Salaam,” amesema Moallin.
Ni kambi ya siku 20 Azam FC itakaa ambapo ipo katika Mji wa El Gouna huku Simba ikiwa imeweka kambi katika Mji wa Ismailia yote ikiwa ni miji ya kitalii nchini Misri.