Mchambuzi wa soka nchini Saleh Ally ‘Jembe’ ameoneshwa kushangazwa na kitendo cha wazee wa klabu ya Yanga kutaka kwenda kuonana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ili kuzungumzia sakata la Msemaji wa klabu hiyo Haji Manara, huku akibainisha kuwa kwa kufanya hivyo hakutasaidia chochote kwani hata Rais Samia pia anaelewa nini maana ya kuheshimu Mamlaka.
Jembe amesisitiza kuwa si kwa sababu tu ni wazee basi wasifuate taratibu na kuheshimu Mamlaka kwani anaamini kumekuwa na kasumba kwa klabu za Simba na Yanga linapotokea tatizo la kinidhamu basi wanatumika wazee kama chambo.
Akiongea katika Kipindi cha Krosi Dongo kinachorushwa na Studio za Global TV na 255 Global Radio Jembe amesisitiza kuwa ipo haja ya wazee wa Yanga kuheshimu Mamlaka za soka nchini.
“Hivi kwani unataka kuniambia hawa wazee wanaruhusu watu wawatukane watu kwasababu wao ni wazee, hawa wazee kwanini wasisisitize procedures zifanyike lakini pia hawa wazeeunataka kuniambia leo wanaenda kuandamana lakini wanampinga hata Waziri mwenye dhamana ya Michezo mwenyewe ambaye amesisitiza mamlaka ziheshimiwe, tufuate sheria kwa mfano kama mimi ni mzee nyumbani kangu kijana hana adabu kwahiyo inatakiwa mimi nimuache afanye lolote tu
Aidha amesisitiza kuwa kwa kitendo cha Wazee kutaka kuonana na Rais Samia ni wazi kuwa wanapingana na maelekezo ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mohamed Mchengerwa aliyetaka watu wote katika tasnia ya michezo kuheshimu Mamlaka zilizopo.