Imepita kama wiki tangu kiungo mshambuliaji wa Simba, Pape Sakho atwae tuzo ya Bao Bora kwenye michuano ya Caf.
Bao la Sakho liliingia kwenye kinyang’anyiro cha michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika akifunga dhidi ya Asec Mimosas Februari 13, mwaka huu katika Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.
Bao hilo alifunga kwa tiktak akimalizia mpira wa krosi tamu ya beki Shomari Kapombe na kumfanya Sakho kubeba tuzo akimbwaga Zouhair El Moutaraji wa Morocco anayeichezea Wydad Casablanca ambaye aliingia naye fainali.
Siku ya tuzo nchini Morocco, Sakho alionekana kuzungumza na nyota wa Bayern Munich, Saido Mane na kocha wa timu ya taifa ya Senegal, Aliou Cisse na nyota huyo amefunguka kwa mara ya kwanza kile alichozungumza na wakali hao.
Katika mahojiano maalumu akiwa nchini Misri ambako Simba imeweka kambi kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya. “Sadio Mane ni nuru yetu na ni mtu mnyenyekevu sana.
Alinipongeza na kunitia moyo kwa kuniambia kuwa naweza kufanya vizuri zaidi, naweza kushinda tuzo aliyoshinda yeye mara mbili. Aliniambia niendelee na kazi na nitoe kila kitu ili kuisaidia timu yangu ya Simba
“Ni mara ya kwanza tulikutana, lakini wakati mwingine tulizungumza kwenye mtandao wa kijamii wa Instagram, kama nilivyosema Sadio ni mtu mzuri na mnyenyekevu sana,” alisema.
Nini alizungumza na kocha Cisse?
Sakho anasema: “Nimebahatika kuongea dakika chache na kocha wa timu ya taifa ya Senegal, Cisse, akanipa ushauri katika maisha ya soka na binafsi. Ni mnyenyekevu na anajua kuisimamia timu…
Lakini siwezi kujua iwapo nitaitwa timu ya Taifa kwa Kombe lijalo la Dunia, sina uhakika ila naomba niwemo kwenda kwenye michuano hiyo ili nitetee rangi za taifa langu.”
Kabla hata ya hiyo tuzo, staa huyo alikuwa anadaiwa kupata ofa mpya nje ya Simba, lakini yeye anafafanua kuwa kwake hilo haliwezi kukosekana ila wakala wake ndiye kila kitu.
“Ni kawaida kupokea ofa au mawasiliano na timu, lakini namuacha wakala wangu alifanyie kazi kwa sababu anaijua kazi yake siwezi kuizungumzia sana.”
Sakho alisema tuzo imemuongezea thamani katika maisha ya soka na alistahili kutwaa na imempa hamasa zaidi kupambana.
“Najivunia kwa sababu nastahili kuwa na tuzo hii na ni hamasa kubwa kuendelea na kazi ambayo nimekuwa nikiwaza kuwashinda wengine. Nawapongeza pia viongozi wa Simba, mashabiki na wachezaji ambao wamekuwa wakinithamini na kunitia moyo kila wakati,” anasema nyota huyo.
“Nawashauri wachezaji wenzangu waendelee na kazi kwani wote wanastahili tuzo hii. Nawashauri wapambane zaidi na watoe kila kitu Mungu anaona kila kitu na kazi pekee ndio inalipa.”
Sakho alizungumzia maandalizi ya msimu ujao baada ya msimu uliopita timu yake kupoteza mataji matatu ya Ngao ya Jamii, Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) akisema: “Simba ni timu kubwa ambayo huwa na wachezaji bora na natumaini tutashinda kila kitu msimu huu Inshaallah ninawaamini wachezaji na tunaweza kufanya hivyo.”
AMTAJA KAPOMBE
Baada ya tuzo na kurejea kambini, jambo alilolifanya Sakho ni kumpelekea tuzo hiyo Kapombe ambaye alimpa pasi ya bao.
Katika hilo, Sakho alisema: “Kapombe ni nahodha. Ni mtu mzuri ambaye ananipa ushauri na utani. Tangu mwanzo wa msimu uliopita kila mara alikuwa akinipigia simu na kuniambia ni jinsi gani tutatafuta suluhu uwanjani ndiyo maana huwa tunasema Kapombe ana tochi kwa maana hunionyesha njia kila wakati.”