Home Habari za michezo HIVI NDIVYO REKODI ZA KIBABE ZILIVYOMLETA OKRAH MSIMBAZI…AFUNGUKA ALIVYOPAMBANA KUFANIKISHA DILI LA...

HIVI NDIVYO REKODI ZA KIBABE ZILIVYOMLETA OKRAH MSIMBAZI…AFUNGUKA ALIVYOPAMBANA KUFANIKISHA DILI LA SIMBA…


REKODI tamu alizonazo kiungo mshambuliaji, Augustine Okrah kutoka Ghana zimembeba Mghana huyo aliyetambulishwa na Simba tayari kwa mashindano ya msimu ujao.

Okrah amesaini Simba kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Bechem United, lakini kabla ya hapo aliwahi kuzichezea timu tofauti kwa mafanikio na rekodi hizo ndizo zilizofanya mabosi wa Msimbazi kumbeba ili aje kuliamsha na wenzake kikosini.

Sifa zake kuu ni uwezo wa kumudu kucheza maeneo tofauti uwanjani ikiwemo kiungo mshambuliaji, mshambuliaji wa pili na wingi zote mbili kulia na kushoto pia anasifika kwa kasi, nguvu na sambamba na kuwa mtaalamu wa kupiga frii-kiki na mashuti ya mbali.

Ujio wa Okrah utamrahisisha Kocha Zoran Maki kwani atakuwa na mabadiliko katika eneo lake la kiungo cha juu ambapo anao wachezaji kama Clatous Chama, Pape Sakho, Peter Banda, Kibu Denis, Yusuph Mhilu, Jimmyson Mwanuke na Moses Phiri aliyesajiliwa kutoka Zambia.

Msimu ulioisha akiwa na Bachem, Okrah alionyesha kiwango bora zaidi na kucheza mechi 32 za ligi akikosa mbili pekee na kufunga mabao 14 na kutoa asisti sita akiisaidia timu kumaliza ligi ikiwa nafasi ya tatu nyuma ya Medeama na Asante Kotoko waliokuwa mabingwa.

Aidha, Okrah alionesha kiwango bora kwenye Kombe la Shirikisho la Soka, Ghana na kufunga mabao manne na kuasisti mara nne.

Kiwango hicho kilimfanya kocha mkuu wa timu ya taifa ya Ghana, Otto Addo kumjumuisha kikosini Okrah katika timu imara yenye mastaa kibao wa dunia kama Thomas Partey, Andre Ayew, Asamoah Gyan, Jordan Ayew, Mohamed Salisu na wengine kibao huku wengi wao wakitokea kwenye ligi kubwa za Ulaya.

Ubora wa Okrah sio wa juzi wala jana kwani amethibisha hilo kila sehemu aliyopita ikiwemo ndani ya miamba ya soka la Ghana, Asante Kotoko, Liberty, Al Merreikh na Al Hilal za Sudan. Okrah amewahi kucheza Ligi Kuu ya Misri katika timu ya Smouha na NorthEast United FC India ya ligi ya India na alisema amekuja Simba kufanya kazi.

SOMA NA HII  ANALIPWA BIL 2 KWA TANGAZO MOJA

“Ni ndoto iliyotimia, nimefurahi sana kujiunga na timu hii kubwa Afrika, jana nimeongea na familia na marafiki zangu, kila mmoja amefurahi na wamenitakia kheri katika msimu wangu wa kwanza Tanzania.

“Haikuwa ngumu kwangu kuchagua kujiunga na Simba, ujue mimi huwa naangalia mbele hivyo niliiona ni klabu yenye malengo makubwa hivyo nikawaambia viongozi wangu waachane na ofa nyingine nijiunge na Simba,” alisema Okrah, huku kiungo wa zamani wa Simba na Yanga, Athuman Iddi ‘Chuji’, alimtaka kusoma mazingira na kujua Simba inachezaje na kutaka nini kutoka kwake kwanza.

“Anatakiwa kuijua Simba vizuri, ajue mbinu, malengo na utamaduni wa timu ile ndio atakuwa bora zaidi, lakini kutokana na wasifu wake anaonekana ni mchezaji mzuri na ataisaidia timu,” alisema Chuji ambaye kwa sasa ni kocha wa Bullet Force inayoshiriki Ndondo.