Home Habari za michezo KOCHA MPYA SIMBA AVUNJA UKIMYA…AFUNGUKA NAMNA VIONGOZI ‘WANAVYOMHENDO’…AANIKA MAKUBALIANO YOTE…

KOCHA MPYA SIMBA AVUNJA UKIMYA…AFUNGUKA NAMNA VIONGOZI ‘WANAVYOMHENDO’…AANIKA MAKUBALIANO YOTE…


Kocha mpya wa Simba, Zoran Manojlovic Maki amevunja ukimya kwa kuzungumza huku akifichua jinsi alivyouchungulia mziki wa timu hiyo mapema na usajili unaoendelea kikosini akiamini msimu ujao mataji yote yaliyotowekwa Msimbazi yatarejea.

Zoran amepewa mkataba wa mwaka mmoja Simba akichukua nafasi ya Pablo Franco aliyetimuliwa, huku timu ikiwa imepoteza mataji matatu iliyokuwa nayo ya Ngao ya Jamii, Ligi Kuu na ASFC.

Mataji hayo yote yamebebwa na Yanga, lakini kocha Zoran akizungumza kwa mara ya kwanza na juzi kwa njia ya simu kutoka Serbia, alisema anaamini mataji hayo yatarudi wakijipanga vyema.

Kocha huyo Mreno mwenye asili ya Serbia, alisema ataungana na kikosi hicho Julai 15 katika kambi itakayowekwa Misri kwa maandalizi ya msimu ujao, kwa vile eneo alililopo (Serbia) na Misri ni karibuni kuliko kama angekuja Tanzania kisha kusafiri tena na timu hiyo kambini.

Zoran alisema amekubaliana na uongozi atatambulishwa kwa wachezaji wapya na waliomaliza msimu pamoja wasaidizi wake wa benchi la ufundi wakiwa kambini kisha aanze kazi ya maandalizi ya timu.

“Tutaanza maandalizi taratibu ili wachezaji wazoee mazingira na kupata nafasi ya kujuana ila kadri siku zitakavyoenda tutaongeza kasi kufanya mengi na magumu yakiwa sehemu kubwa ya maandalizi kabla ya kucheza mechi za kirafiki,” alisema Zoran na kuongeza;

“Tunafanya hivyo kwa vile pre-season ni sehemu muhimu ya kuandaa wachezaji katika utimamu wa miili na kushindana, kama tutafanikiwa hapa maana yake tutakwenda kufanya vizuri.”

Zoran aliyewahi kuzinoa timu kama Primeiro do Agosto ya Angola, Wydad Casablanca ya Morocco na Al Hilal ya Sudan, alisema licha ya ugeni Simba, lakini amekuwa akiifuatilia timu hiyo na kuwasoma wachezaji kupitia runinga.

“Nikiwa ndani ya timu nitapata muda wa kufahamu zaidi wachezaji na sifa zao, hii tofauti na wakati huu nimekuwea nawaona kupitia runinga, ila nikiri wengi wao wana vipaji vikubwa na waelewa. Tumaini langu tukiungana, tutafikia malengo ya klabu,” alisema Zoran na kuongeza;

“Baada ya kukubaliana na Simba, nimekuwa nikipata ushirikiano mzuri kutoka kwa viongozi na kushauriana katika mambo ya kimsingi, haswa yale yanahusu ufundi.

SOMA NA HII  ALICHOSEMA MAMA AKE MKUDE..BAADA YA MWANAE KUPIMWA AKILI

“Malengo yangu ni kuhakikisha msimu ujao unakuwa bora tofauti na sasa tulioshindwa kutwaa taji lolote katika mashindano ya ndani, naamini hilo kwa ushirikiano huu linawezekana.”

Alisema anajua kiu ya mashabiki wa Simba ni kuona timu inarejesha mataji iliyopoteza, pia kufikia malengo aliyowekewa na mabosi wake.

“Baada ya kambi, nikirejea Tanzania nitakuwa na mengi ya kueleza tofauti na ilivyo sasa, ila ukweli nimekuja Simba na nia ya kuipaisha timu mahali ilipo,” alisema Zaron aliyeifikisha Primeiro de Agosto nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa na kuifikisha Wydad makundi pamoja na robo fainali ya Mabingwa Afrika.