Home Habari za michezo KUELEKEA MSIMU UJAO…NABI ARUDI NA MAFAILI MATATU YANGA…MWINYI ZAHERA AFUNGUKA ISHU YA...

KUELEKEA MSIMU UJAO…NABI ARUDI NA MAFAILI MATATU YANGA…MWINYI ZAHERA AFUNGUKA ISHU YA KAMBI KIGAMBONI…


Mastaa wa Yanga wamerejea kambini jana kuanza maandalizi ya msimu mpya lakini benchi la ufundi chini ya kocha Nasreddine Nabi wana siri nzito kwenye mafaili yao.

Kazi ya kwanza ni kuwaimarisha kimbinu, kiufundi na kifiziki wawe tayari kuhimili ushindani lakini pili ni kumaliza sintofahamu ya mikataba yao ya kazi ambayo huenda wakasaini muda mfupi baada ya kuwasili kutegemeana na uharaka wa mazungumzo.

Lakini jambo la tatu kubwa ambalo ni siri kubwa ya Nabi na wasaidizi wake ni kutoa uamuzi wa mpangilio wa kikosi hasa kwa nyota wa kigeni katika msimu ujao kutokana na ujio wa wachezaji wapya.

Tayari wameshachukua uamuzi kumtema Chico Ushindi na kumtoa kwa mkopo Songne Yacouba, kibarua kigumu ambacho kipo mbele yao kwa sasa ni mkakati wa kupata nyota nane wa kigeni ambao watakuwa tegemeo katika kikosi chao msimu ujao kulingana na matakwa ya kikanuni.

Kwa mujibu wa kanuni ya idadi ya wachezaji wanaopaswa kutumika katika mchezo mmoja, kila timu inaruhusiwa kusajili wachezaji 12 wa kigeni lakini itawatumia wachezaji nane tu katika mchezo mmoja na wanaobakia ni lazima wawe wazawa.

Kanuni hiyo inaacha vita kwa nyota 12 wa kigeni ambao wamebakia katika kikosi cha Yanga, kupigania nafasi ya kutumika katika mchezo mmoja ambayo itaamriwa katika kambi hiyo ya maandalizi ya msimu ambayo itafanyika Avic Town, Kigamboni, Dar es Salaam.

Wachezaji hao 12 wa kigeni ambao wamebakia ni Bernard Morrison, Jesus Moloko, Fiston Mayele, Djuma Shaban, Yannick Bangala, Djigui Diarra, Ki Aziz, Joyce Lomalisa, Heritier Makambo, Khalid Aucho, Lazarous Kambole na Gael Bigirimana.

Ingawa kambi hiyo ya maandalizi itakuwa na nafasi kubwa ya kutoa hatima ya wageni wanane ambao watajihakikishia nafasi katika kikosi cha kwanza, wapo wachezaji ambao wamejiweka katika nafasi nzuri.

Kiwango bora cha ambacho Mayele alionyesha katika viwanja tofauti msimu uliopita pasipo kujali ubora wa eneo la kuchezea, kina nafasi kubwa ya kumpa nafasi kama ilivyo kwa kipa Diarra.

Ukiondoa hao, kuna Yannick Bangala aliyeibuka mchezaji bora wa Ligi Kuu msimu uliomalizika ambaye uwezo wa kucheza nafasi nyingi tofauti uwanjani hasa za ulinzi, unaweza kuwa silaha tosha ya kumshawishi Nabi aendelee kumfanya mchezaji tegemeo kikosini.

Nyota wengine ambao wanaweza kuwa na nafasi kubwa ni beki wa kulia Djuma Shaban ambaye alikuwa kinara wa kupiga pasi za mwisho katika msimu uliomalizika kama ilivyo kwa kiungo wa kati Aucho.

SOMA NA HII  MWAMBUSI: TUTAFANYA VIZURI NDANI YA LIGI NA KOMBE LA SHIRIKISHO

Gharama kubwa ya fedha iliyotumika kumnasa Stephane Aziz Ki inaweza kumbeba kikosini lakini shughuli pevu huenda ikabakia kwa Morrison, Moloko, Kambole, Makambo, Lomalisa na Bigirimana ambao kati ya hao, wanne watajikuta wakikaa jukwaani huku wawili tu ndio watapeta.

Lomalisa anayecheza nafasi ya beki wa kushoto, anapaswa kuonyesha kitu katika maandalizi ya msimu ili amshawishi Nabi ampe nafasi mbele ya mzawa, Kibwana Shomari ambaye alikuwa tegemeo msimu uliomalizika.

Bigirimana aliyewahi kuchezea Newcastle ya England, ana kibarua cha kuhakikisha anamudu vyema mazingira na kuonyesha kiwango kizuri ambacho kitamshawishi Nabi asimtumie ama Aucho au Bangala na kumhakikishia nafasi yeye.

Uwepo wa nyota wengi wazuri katika nafasi ya ushambuliaji wakiwemo wazawa, unampa kibarua Nabi cha kuchuja kati ya Morrison, Moloko, Kambole na Makambo ambao wamebakia kuchuja nani atakuwa miongoni mwa nane wa kucheza na watakaogeuka watazamaji.

Lakini sio tu nyota hao wa kigeni ambao watampasua kichwa, Nabi mazoezini bali hata wale wazawa katika kuamua nani wa kutumika katika mechi na wale wa kujaza nafasi mazoezini.

Wachezaji 18 watakuwa na kibarua cha kugombania nafasi 10 za kutumika katika mechi za mashindano ya ndani msimu ujao huku wengine nane wakibaki kuwa watazamaji wa wenzao. Kiwango na kutumika kwao msimu uliopita, vinatoa taswira kuwa wachezaji, Dickson Job, Kibwana Shomari, Bakari Mwamnyeto, Farid Musa, Abuutwalib Mshery, Salum Abubakar, Feisal Salum, Dickson Ambundo, Denis Nkane na Ibrahim Baka watakuwa na nafasi kubwa ya kuwemo katika vikosi vya mechi vya Yanga.

KAMBI YA AVIC

Mkurugenzi wa Maendeleo ya Soka la Vijana, Mwinyi Zahera alipongeza hatua ya Yanga kuamua kuweka kambi Avic Kigamboni. “Msimu uliopita Yanga ilikwenda Morocco lakini hawakupata muda sahihi wa kujiandaa walirudi na maandalizi yao mengi waliyafanyia hapohapo Avic na wakashinda makombe yote hii inatakiwa kuwa elimu, walizishinda timu zilienda Zambia na hata Morocco,” alisema Zahera na kuongeza;

“Kama wachezaji watabaki hapa wakajiandaa vizuri, unaweza kutumia siku kama moja unawapa nafasi ya kurudi kuona familia zao na wanarudi tena kujiandaa hii itawasaidia kuwafanya akili zao kutulia zaidi na kupambana.

Nabi pia anataka kuongeza wataalamu wawili kwenye benchi lake la ufundi.