Home Habari za michezo KUELEKEA MSIMU UJOA…NI PATASHIKA NGUO KUCHANIKA KATI YA YANGA,SIMBA, AZAM NA GEITA…MAMBO...

KUELEKEA MSIMU UJOA…NI PATASHIKA NGUO KUCHANIKA KATI YA YANGA,SIMBA, AZAM NA GEITA…MAMBO LAZIMA YWE MAGUMU…


Huko mtaani kwa sasa kuna kelele nyingi juu ya sajili zilizofanywa na klabu za soka nchini hususani Simba, Yanga, Azam na hata Geita Gold.

Kila upande umekuwa ukivutia upande wake na wengine kwenda mbali wakitamba kama vipi Ligi Kuu Bara ianze hata sasa watu waumizane uwanjani.

Tambo hizo zimechangiwa zaidi na aina ya wachezaji waliosajiliwa na klabu hizo, Yanga wakitambia kina Stephane Aziz KI, Lazarous Kambole, Joyce Lomalisa na Bernard Morrison aliyerejea kutoka Msimbazi, huku Simba ikitamba na kina Nelson Okwa, Moses Phiri, Augustine Okrah na Mohammed Ouattara, huku Azam ikitambia bonge la kipa, Ahmada Ali, Kipre Junior na Abdul Suleiman ‘Sopu’.

YANGA

Mabingwa hao wa nchi juzi walimshusha Mbukinabe Aziz KI akitokea Asec Mimosas ya Ivory Coast akiungana na Mghana Morrison aliyetoka Simba, Mrundi Gael Bigirimana aliyewahi kukipiga Newcastle, Lomalisa na Kambole kutokea Kaizer Chiefs.

Kuingia kwa wachezaji hao kukutana na wale waliokuwapo msimu uliopita umewavimbisha kifua wanayanga wanaoamini ule moto wa Unbeaten utaendelea tena msimu unaoanza Agosti 13 kwa mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Simba.

Kwa usajili huo, ni wazi kikosi cha Nasreddine Nabi kitabadilika na huenda kikawa bora zaidi na kutisha Afrika nzima.

Mashabiki wanatamani mziki wao upangwe hivi; langoni Djigui Diarra, huku Djuma Shabani na Lomalisa wakicheza mabeki wa pembeni, kati Bakar Mwamnyeto na Yanick Bangala na Viungo wacheze wanne, chini akisimama Bigirimana na Khalid Aucho, huku Morrison na Aziz Ki wakicheza pembeni na kati kutakuwa na Fiston Mayele na Feisal Salum ‘Feitoto’ kama washambuliaji, kitatisha.

Huko nje kuna vyuma vingine vya hatari, Aboutwalib Mshery, Kibwana Shomary, Kambole, Dickson Job, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Chico Ushindi na Heritier Makambo, japo klabu hiyo inatakiwa kupunguza mchezaji mmoja wa kigeni ili kwenda na kanuni ya usajili ya Ligi Kuu.

Yanga kwa sasa ina nyota 13 akiwamo Jesus Moloko anayedaiwa huenda akatolewa kwa mkopo.

SIMBA

Mnyama naye kikosi kizima nje mtiti, ndani mtiti licha ya kuwepo kwa utata wa kuwa na nyota 14 wa kigeni akiwamo, Cesar Manzoki ambaye dili lake bado lina utata, ikitakiwa kupunguza majembe mawili ili kubaki na wachezaji 12 kama kanuni inavyotaka.

Hata hivyo, mziki wa Simba nao si mchezo kwani imeongeza nyota watano wa kigeni Mnigeria Victor Akpan kutokea Coastal Union, Mzambia Phiri aliyekuwa Zanaco, Mghana Okrah kutokea Bechem, Mbukinabe Ouattara kutoka Al Hilal, Mganda Ceser Manzoki kutoka Vipers huku wazawa wakiwa Habib Kyombo kutoka Mbeya Kwanza na kiraka Nassoro Kapama aliyekuwa Kagera Sugar.

Wote hao huko walikotoka wamefanya makubwa na baadhi yao tayari wamejiunga na timu nchini Misri ilipojichimbia kambi kwa ajili ya msimu ujao ‘Pre Season’.

Mastaa hao lazima wapangue kikosi cha Simba cha msimu uliopita na kuifanya iwe imara zaidi ndani na nje ya nchi hususani katika Kombe la Shirikisho Afrika ilikoweka malengo ya kufika nusu fainali.

SOMA NA HII  MSUVA AWAKANA YANGA...SIMBA NI KLABU KUBWA AFRIKA...INAFANYA VIZURI LIGI YA MABINGWA

Kikosi cha Simba msimu ujao huenda kikawa hivi; Aishi Manula, Mohamed Hussein Tshabalala na Shomari Kapombe kama mabeki wa pembeni huku kati ni Ouattara na Henock Inonga, wakati eneo la kiungo chini atakuwa Akpan na juu watasimama mafundi watatu, Okrah, Clatous Chama na Pape Sakho na pale mbele watamaliza Okwa na Phiri.

Nje kuna vichwa vingine akiwamo Manzoki, Beno Kakolanya, Israel Mwenda, Joash Onyango, Sadio Kanoute, Peter Banda, Kibu Denis, Chris Mugalu na John Bocco.

AZAM

Matajiri wa Chamazi raundi hii hawataki utani kabisa na bosi mkubwa, Yusuf Bakhresa ameingilia usajili na hadi sasa ameshusha wageni watano wa maana na wazawa watatu hatari.

Isah Ndala kutoka Plateau ya Nigeria, Tape Edinho na Kipre Junior wote wa Ivory Coast, Ahmada kutoka Comoro na Mghana James Akaminko kutoka Great Olympic ni wageni walioshushwa hadi sasa huku wazawa wakiwa Nathanael Chilambo kutokea Ruvu Shooting, Cleophace Mkandala kutoka Dodoma Jiji na Sopu kutoka Coastal Union na sasa ipo mbioni kukamilisha usajili wa mwisho kwa kushusha beki hatari.

Mastaa hao wakiungana na wale waliokuwepo msimu uliopita, chama hilo chini ya Kocha Abdihimid Moallin litabadilika na huenda likawa hivi;

Ahmada ndiye atasimama langoni na beki ya kulia atamaliza Chilambo wakati kushoto akicheza Kangwa na kati watasimama Daniel Amoah na Aggrey Morris, japo bado wanasikiliza beki mwingine mkali zaidi wa kimataifa kufungia usajili wao.

Viungo wawili wa chini watacheza Ndala na Akaminko huku juu yake wakitawala mafundi watatu, Sopu, Kipre na Edinho na pale mbele atamaliza Rogers Kola.

Benchi hapo unawakuta kina Wilbol Maseke, Abdalah Sebo, Sospeter Bajana, Keneth Muguna, Idris Mbombo, Iddi Nado na Prince Dube.

GEITA NAO

Ikiwa ni msimu wa kwanza Ligi Kuu, Geita Gold ilikiwasha na kumaliza nafasi ya nne kwenye msimamo ikikata tiketi ya kucheza Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza.

Ili kuhakikisha inafanya vizuri na kuendeleza ubabe kama ilivyokuwa msimu uliopita, Geita imeongeza mastaa ndani ya kikosi chake kwa kumvuta mgeni, Yacouba Sogne kutoka Yanga na wazawa Ramadhan Chombo ‘Redondo’ aliyekuwa Biashara, Seleman Ibrahim ‘Boban’ kutoka Mbeya City na Yahya Mbegu kutoka Polisi Tanzania.

Maingizo hayo huenda yakakiboresha zaidi kikosi cha Geita na msimu ujao kikawa kinaanza hivi;

Kipa atakuwa Khomeiny Abubakar, Mbengu atacheza beki ya kulia wakati kushoto akimaliza David Kameta ‘Duchu’ na kati watasimama wakongwe Juma Nyosso na Kelvin Yondani.

Viungo watacheza watatu, Kelvin Nashoni, Redondo na Boban na mbele watacheza watatu, Mpole katikati huku Yacouba na Danny Lyanga wakitokea pembeni kwenye mfumo wa 4-3-3.

Hapo nje kutakuwa na kina Aaron Karambo, Adeyum Saleh, Edimund Massota, Maka Edward, Juma Mahadhi na mastaa wengine. Usipime.