Home Habari za michezo KUTOKA KUTANIWA KUWA NI WANAMUZIKI…HIVI NDIVYO WACONGO WALIVYOIBEBA YANGA KWENYE UBINGWA MSIMU...

KUTOKA KUTANIWA KUWA NI WANAMUZIKI…HIVI NDIVYO WACONGO WALIVYOIBEBA YANGA KWENYE UBINGWA MSIMU HUU…


WALIANZA kwa kutaniwa, Yanga imesajili wanamuziki kutoka Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Hii ni kutokana na historia ya taifa hilo kwenye muziki wa Lingala ulio maarufu hapa nchini na duniani kwa jumla. 

Mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara walisajili wachezaji watano na kufanya uwepo wao kuwa sita wakiungana na Mukoko Tonombe ambaye alikuja msimu mmoja kabla na aliuzwa TP Mazembe na nafasi yake kuzibwa na Chico Ushindi aliyejiunga na timu dirisha dogo la usajili.

Ni wazi, ukitaja mafanikio ya Yanga msimu huu, huwezi ukaacha wacongo hawa ambao katika kila nafasi zao uwanjani, wamefanya makubwa.

Hii hapa orodha ya mastaa hao ambao viwango vyao vimewaziba midomo waliokuwa wakibeza usajili wao baada kuipa taji la Ligi Kuu Yanga ambayo leo inashuka Uwanja wa Benjamin Mkapa kumaliza msimu dhidi ya Mtibwa Sugar mchezo utakaoanza saa 10:00 jioni.

FISTON MAYELE

Ndiye kinara wa mabao Yanga na Ligi Kuu akivalia jezi namba tisa baada ya kutambulishwa rasmi mwezi Agosti Mosi, mwaka jana.

Mabao yake hayo yameisaidia Yanga kumaliza msimu ikiwa kileleni na kuwa kipenzi cha mashabiki.

Alisaini mkataba Yanga akitokea AS Vita ya Congo alikomaliza akiwa nafasi ya pili kwa ufungaji akiwa nayo 13 na akiwa Yanga msimu huu sasa ameichezea michezo 29, akihusika na mabao 21 Ligi Kuu (amefunga mabao 16 na asisti 5).

DJUMA SHABAN

Djuma ni miongoni mwa mabeki bora na tegemeo kwenye kikosi cha timu ya taifa ya DR Congo na anasifika kwa kukaba na kupandisha mashambulizi.

Amethibitisha hilo pia akiwa na Yanga na kutengeneza ufalme kwenye nafasi yake akisaidiana na wazawa Dickson Job, Bakari Mwamnyeto na Kibwana Shomari.

Ujio wa Djuma umekuwa mwiba kwa wazawa David Bryson, Yassin Mustafa ambao wameshindwa kuingia moja kwa moja kikosi cha kwanza baada ya nafasi hiyo kuchukuliwa na Kibwana ambaye waliyebadilishana namba na Djuma.

Beki huyo amehusika kwenye mabao saba ya Yanga akifunga mawili na asisti tano.

SOMA NA HII  MUONEKANO WA UKURASA WA MBELE GAZETI LA CHAMPIONI JUMATANO

JESUS MOLOKO

Haimbwi sana midomoni mwa mashabiki wa Yanga kama ilivyokuwa kwa Tuisila Kisinda ambaye aliuzwa na Yanga Morroco kwenye timu ya RS Berkane.

Hata hivyo, nafasi yake alizibwa na Moloko ambaye pamoja na kushindwa kuonyesha kiwango kilichokuwa kinatarajiwa amekuwa na mchango ndani ya timu.

Moloko nafasi yake amekuwa akibadilishana na Job, Farid Mussa na tofauti na wacongo wengine, hajacheza michezo mingi lakini ni kati ya mastaa wa Congo waliohusika kwa namna moja au nyingine kuibeba Yanga msimu huu na kuipa taji la 28 la Ligi Kuu Bara.

YANICK BANGALA

Kiraka ambaye amekuwa na msaada ndani ya Yanga tangu ametua ndani ya kikosi hicho.

Amecheza nafasi mbili tofauti akianza kama kiungo mkabaji akisaidiana na Khalid Aucho na wakati mwingine ametumika kama beki wa kati akicheza sambamba na nohodha wao, Bakari Mwamnyeto.

Hatajwi sana ila msimu huu ameonyesha uwezo mkubwa na kuifanya Yanga hadi sasa kuwa imeruhusu mabao machache zaidi ya kufungwa (nane) na anatajwa mmoja wa wachezaji bora wa msimu kutokana na ubora wake.

MAKAMBO/USHINDI

Hawajawa na msimu mzuri lakini kwa kiasi chake, wamekuwa kati ya wacongo walioipa Yanga ubingwa wa Ligi Kuu Bara.

Wakati Heritier Makambo akisajiliwa dirisha kubwa la usajili mwaka jana, Ushindi alijiunga na Yanga dirisha dogo akitokea TP Mazembe.

Makambo amefunga mabao mawili hadi sasa Yanga ikisaliwa na mchezo mmoja unaopigwa leo, huku Ushindi akifunga bao moja.

Ni kutokana na kukosa nafasi ya kucheza mbele ya Mayele ambaye amekuwa chaguo la kwanza la Nabi kutokana na mfumo wake wa kutumia mshambuliaji mmoja.

Hata hivyo, wanasubiriwa kama msimu ujao watakuwepo kuona kama wataonyesha viwango vyao.