Yanga imeendelea na maandalizi yake kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu Bara ikiwa inashikilia mataji matatu iliyotwaa msimu uliopita, huku ikiwa na moto.
Mafanikio hayo Yanga wataanza kuyatetea kuanzia Agosti 13 watakapokutana na Simba katika mchezo wa ufunguzi wa msimu – ule wa Ngao ya Jamii ambayo walianza nayo mapema msimu uliopita wakiwafunga watani wao hao.
Hata hivyo, nyuma ya Yanga kuna mitego mitano ambayo itamlenga kocha Nasreddine Nabi ambaye ndiye aliyeongoza jahazi hilo la mabingwa hao kuhakikisha kila kitu kinakuwa freshi kwao.
KUTETEA MATAJI
Yanga ilichukua Ngao ya Jamii msimu ulipita, ikitwaa pia taji la Ligi Kuu Bara na mwisho ikamalizia Kombe la Shirikisho la Azam wakimaliza pia msimu bila kupoteza mchezo wowote. Mafanikio hayo yatakuwa na swali moja tu kwa Nabi, kama ataweza kuthibitisha ubora huo kwa kuchukua tena makombe hayo msimu ujao.
Msimu ujao wa ligi unatabiriwa kuonekana kwamba utakuwa mgumu kutokana na klabu nyingi kujipanga sawasawa na hilo litailazimu Yanga ya Nabi kuwa na ubora zaidi ya ule msimu uliopita kulinda mafanikio yao msimu huu.
LIGI YA MABINGWA
Msimu uliopita pia Nabi aliiongoza Yanga kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini kwa mshtuko mkubwa timu hiyo iliondolewa katika hatua ya awali wakipoteza mechi zote mbili za nyumbani na ugenini kwa kufungwa bao 1-0 kila mchezo na Rivers United ya Nigeria.
Hatua hiyo iliwashangaza wengi ingawa kulikuwa na sababu nyingi ambazo ziliilazimisha Yanga kufikia anguko hilo. Hata hivyo, msimu ujao Yanga itarejea tena Ligi ya Mabingwa Afrika na kwa kikosi ilichonacho msimu huu kinamfanya Nabi kubaki na deni la kuthibitisha ubora katika mashindano hayo.
WAGENI WANANE
Mtego mwingine mgumu kwa Nabi ni juu ya wachezaji 12 wageni alionao katika kikosi chake ambao kwa majina wanaonekana kuwa bora na kila mmoja atahitaji nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza.
Iko hivi, kanuni za Ligi Kuu Bara zinamtaka Nabi kuanza na wachezaji wanane tu kati ya 12 na mtego unakuja atamchagua nani na atamuweka nani nje hasa ikitokea kila mchezaji anajiona yuko fiti.
Mastaa wa kigeni alionao Nabi ni kipa Diarra Djigui; mabeki Djuma Shaban, Joyce Lomalisa na Yannick Bangala ilhali viungo ni Khalid Aucho, Gael Bigirimana, Stephane Aziz KI, Jesus Moloko na Bernard Morrison hukuwa washambuliaji wakiwa ni Lazarous Kambole, Heritier Makambo na Fiston Mayele. Nabi hapo atatakiwa kuchagua wasiozidi wanane kwa kila mchezo.
UKUTA SASA
Kuna mabeki wawili wa kati wazawa wa Yanga, nahodha Bakari Mwamnyeto na Dickson Job ambao msimu uliopita walicheza pamoja pale kati kwa muda mrefu. Lakini hapa kutakuwa na mtego mwingine kwa Nabi kutokana na kuingia katika uhitaji wa kuchagua mmoja kati ya hawa kuanza nao.
Utata mwingine ni kwamba mabeki hao ndio pia wanaibeba timu ya taifa ‘Taifa Stars’ na Nabi atahitaji kuwa na beki wa kati imara katika mashindano ya ndani na nje akitafuta nafasi ya Bangala ambaye anaweza kucheza eneo la beki wa kati na hata kiungo.
VIWANGO VYA WACHEZAJI
Msimu uliopita Yanga ilifanikiwa kutokana na wachezaji wengi kuwa katika viwango bora ambapo licha ya wakati flani kukumbwa na janga la majeruhi, lakini Nabi aliwaimarisha nyota wengine kuziba nafasi zao vyema.
Mtego utakuja msimu ujao na hilo ataliweza kulifanya kama alivyofanya msimu uliopita kwa mafanikio? Kama atayashindwa haya au mojawapo kuna uwezekano mkubwa timu hiyo ikaanza kupepesuka kutokana na utofauti wa ubora wa mastaa wake waliokuwepo msimu uliopita kukosa mwendelezo wa viwango katika msimu ujao. Hata hivyo ni suala la kusubiri na kuona.