Kocha wa Simba, Zoran Maki amesema ratiba ya Ligi Kuu Bara imekuwa rafiki kwao kutokana na kucheza mechi tatu za kwanza katika uwanja wa nyumbani ambao upo na mazingira mazuri haswa eneo la kuchezea.
Zoran amesema wanatakiwa kuanza vizuri katika mechi hizo kwa kukusanya pointi zote tisa ili ikianza ratiba ya kucheza mechi za ugenini wanakupa na kitu wamekifanya tayari.
Amesema kuanza Ligi kwa kupata ushindi katika mechi tatu za awali maana yake watakuwa wametengeza morali kubwa kwa wachezaji wake hata wakitoka katika mechi za nje.
“Ukiangalia msimu uliopita miongoni mwa sababu iliyochangia Simba kushindwa kufanya vizuri kutopata matokeo mazuri katika mechi nyingi za nyumbani kama ilivyokuwa kwa wapinzani wao,” amesema Zoran na kuongeza;
“Kwahiyo katika hizi mechi tatu za nyumbani tutaweka mipango ya kupata ushindi na hilo linawezekana kutokana na maandalizi mazuri waliyopata wachezaji,”
“Ukiangalia aina ya timu ambazo tunakwenda kukutana nazo ni nzuri na naamini zitatupa ushindani wa kutosha, tunaelewa hilo na tupo tayari kupambana nalo.”
Katika mechi tatu za awali kwenye Ligi Kuu Bara Simba itaanzia nyumbani dhidi ya Geita Gold, Kagera Sugar na KMC.