Aliyekuwa msemaji wa Yanga SC, Haji Sunday Manara kwa mara nyingine, amemuomba radhi Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa.
Manara ameomba msamaha huo kupitia ukurasa wake wa Instagram ambapo amejirekodi kipande cha video ambacho kinamuonesha akiomba radhi kwa Waziri Mchengerwa pamoja na wizara ya michezo.
“Siku kadhaa zilizopita nilitoa kauli ambayo haikuwa nzuri kwa waziri wetu mwenye dhamana ya michezo Mheshimiwa Mohamed Omary Mchengerwa, nakiri kukosea, naomba radhi kwake binafsi, naomba radhi kwa wizara ya michezo pamoja na Serikali kwa ujumla nilikosea na nakiri makosa na ninaomba msamaha kwa waziri wetu wa michezo Mohamed Mchengerwa,” alisema Manara.
Hivi karibuni, Manara alifanya mkutano na wanahabari ambapo alinukuliwa akimtaja Waziri Mchengerwa kusikika akishinikiza TFF wasimamie misingi ya sheria na kanuni na kutoa adhabu kali kwa wale wanaokiuka maadili na kudharau viongozi wanaosimamia tasnia ya michezo.
Haji alisema, kitendo cha waziri kutamka maneno hayo kwenye usiku wa tuzo za wanamichezo ndicho kilipelekea kamati ya maadili kumpa adhabu kali ya kifungo cha miaka miwili na faini ya milioni 20 jambo ambalo si sahihi.
Katika sakata hilo, Haji amejikuta akiomba radhi mara mbili kwa nyakati tofauti. Alifanya hivyo kupitia kituo cha EFM na usiku wa kuamkia leo aliposti video hiyo mpya akiomba tena msamaha.