Droo ya mechi za hatua ya awali Ligi ya Mabingwa Afrika imefanyika muda mchache uliopita huku Vilabu vya Simba na Yanga vinavyokwenda kuiwakilisha Tanzania katika michuano hiyo, wakifahamu vibarua vigumu wanavyokwenda kukutana navyo katika hatua hiyo.
Yanga ambao ndio Mabingwa wa Ligi Kuu msimu uliopita wataanzia safari yao ugenini dhidi ya klabu ya Zalan FC kutokea Sudan ya Kusini na mshindi baina yao atakutana na mshindi kati ya St George ya Ethiopia dhidi ya Al Hilal ya nchini Sudan katika hatua inayofuata( Raundi ya pili).
Kwa upande wa Simba wao watakuwa ugenini nchini Malawi kukipiga dhidi ya Nyasa Big Bullets ya nchini humo katika hatua ya awali na mshindi wa mchezo huo atakutana na mshindi baina ya Red Arrows ya nchini Zambia ambae atacheza na Primera de Agosto kutoka Angola.
Michezo ya mkondo wa kwanza hatua hiyo ya awali inatarajiwa kupigwa kati ya tarehe 9,10,11 mwezi Septemba, na michezo ya marudiano inatarajiwa kupigwa kati ya tarehe 7,8 na 9 Mwezi Oktoba.