Kocha Mkuu wa Singida Big Stars, Hans van der Pluijm amesema wachezaji wake wapya kutoka Brazil wameanza kuzoea mazingira nchini.
Pluijm alisema kumekuwa na matokeo chanya juu yao huku akiamini kiwango walichokionyesha kwenye mchezo wa kirafiki na Zanaco FC katika tamasha la Klabu hiyo lililofanyika Agosti 4 kimewaongezea hali ya kujiamini.
“Sehemu walizotoka na huku ni tofauti hivyo lazima waanze taratibu ili kuendana na hali halisi, ni wachezaji wazuri ambao naamini katika kikosi changu wameongeza kitu muhimu ambacho kitatusaidia,” alisema Pluijm.
Mtendaji Mkuu wa Klabu hiyo, Dismas Ten alisema mastaa hao wanapewa sapoti na mahitaji ya kutosha kama ambavyo walikuwa wanapata sehemu walizotoka kwa lengo la kuhakikisha ufanisi wao wa kazi unakuwa ni mkubwa.
Wachezaji hao kutoka Brazili waliosajiliwa na timu hiyo kwa ajili ya msimu ujao unaotarajiwa kuanza rasmi Agosti 17 ni, Dario Frederico, Bruno Gomes, Joao Oliviera na Peterson Cruz huku wakitabiriwa kufanya mambo makubwa.
Nyota hao wanaungana na Aziz Andambwile, Paul Godfrey ‘Boxer’, Kelvin Sabato, Abdulmajid Mangalo, Metacha Mnata, Said Ndemla, Benedict Haule, Yassin Mustapha, Pascal Wawa, Deus Kaseke, Khomeiny Aboubakar na Meddie Kagere ‘Terminator’.