Mabosi wa Simba bado wanakumbuka walichokumbana nacho msimu uliopita kwenye mechi ya Ngao ya Jamii na hata katika Ligi Kuu Bara na Kombe la ASFC baada ya watani wao, Yanga kuwazidi ujanja, lakini safari hii wametamba lazima kitaeleweka wikiendi hii.
Simba inatarajiwa kuivaa Yanga kwenye Ngao ya Jamii ikiwa na kumbukumbu ya kulala bao 1-0 msimu uliopita kwenye mechi kama hiyo na mabosi wake wamesema kwa maandalizi waliyofanya hadi sasa wanaamini wikiendi hii watani wao hawatachomoka.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya klabu ya Simba, Salim Abadallah ‘Try Again’ alisema wanaamini kwa kikosi walicho nacho na aina ya wachezaji waliopo mchezo huo wanatoboa kabla ya kugeukia Ligi Kuu Bara na michuano ya kimataifa.
Alisema wanatambua dabi ni mchezo mgumu kutokana na upinzani unaokuwepo kwa pande zote mbili ila kikosi chao wamekiandaa vilivyo kukabiliana dakika zote.
“Msimu uliopita tulipoteza mchezo wetu wa ufunguzi na wao, ilikuwa sehemu ya mchezo tukajikuta tunapoteza mataji yetu yote,” alisema Try Again na kuongeza:
“Kwa sasa tumedhamilia haswa kuanzia Jumamosi kuyarejesha mataji yetu tuliyotamba nayo misimu minne mfululizo, kikosi tunacho na ndio maana tumetoa mtu tukaweza mtu.”
Mshambuliaji wa timu hiyo, Moses Phiri alisema licha ya siku hiyo kuwa dabi yake ya kwanza, anaamini kwa jitihada za timu nzima na juhudi binafsi ya kila mchezaji watafanya vizuri.
“Mashabiki wa Simba waje tu kwa wingi sisi wachezaji tupo kwa ajili yao na tutahakikisha tunapambania ushindi, niliwaona siku ya Simba day nilifurahi sana,” alisema Phiri.