Home Habari za michezo KUELEKEA DABI YA NCHI LEO….FAHAMU UBORA NA UDHAIFU WA SIMBA NA YANGA…ATAKAYEWAHI...

KUELEKEA DABI YA NCHI LEO….FAHAMU UBORA NA UDHAIFU WA SIMBA NA YANGA…ATAKAYEWAHI KAMALIZA KAZI MAPEMA..


Baada ya kufanya sajili za maana kwa pande zote mbili, miamba ya soka nchini Simba na Yanga leo inashuka kuonyeshana ubabe huku kila mmoja akitambia majembe yake mapya.

Mechi ya leo ya Ngao ya Jamii kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam ni ishara ya ufunguzi wa msimu mpya, ambao pamoja na mashindano ya ndani, timu hizo zitaiwakilisha nchi kimataifa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

Katika matamasha yao, Wiki ya Mwananchi, Yanga ilikumbana na kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa mabingwa Uganda, Vipers FC wakati Simba ilishinda 2-0 dhidi ya mabingwa wa Ethiopia, St George katika Tamasha la Simba Day Jumatatu.

Mijadala ya mashabiki kwenye mitandao ya kijamii na kila kona ni uimara wa vikosi vipya vilivyosukwa na kila timu na mambo yatakavyokuwa watakapokutana.

Je, matokeo ya mechi hizo za kirafiki zinabeba tafsiri gani katika mechi za ushindani kwa kuanzia na hii ya Ngao ya Jamii?

Safu za ulinzi za Simba na Yanga zimebadilika kutokana na usajili mpya uliofanyika kwenye dirisha kubwa la usajili linalotarajiwa kufungwa Agosti 30 mwaka huu, zinaweza kuwa na kazi kubwa ya kufanya pale timu hizo zitakapokutana kutokana na ubora wa nyota wanaocheza katika safu za ushambuliaji kwa kila upande.

Usajili uliofanywa katika dirisha hili linaloendelea kila timu imeongeza nguvu huku Simba ikionekana kusajili wachezaji wengi zaidi kuliko watani wao Yanga ambao wameongeza wachezaji watano.

Kutokana na usajili wao wa awamu hii, mabeki wanne watakaounda safu ya ulinzi ya Simba wanaweza kuwa Shomary Kapombe, Mohamed Hussein, Mohammed Ouattara na Henock Inonga β€˜Varane’.

Wanne hao pale watakapokutana na Yanga huenda wakawa na shughuli pevu mbele ya safu ya ushambuliaji ya watani wao ambayo inaweza kuundwa na Bernard Morrisson, Stephane Aziz Ki, Fiston Kalala Mayele na Heritier Makambo.

Varane na Ouattara wanaocheza nafasi ya mabeki wa kati, wao watakuwa na kazi ya kuhakikisha Makambo na Mayele hawafui dafu na kuzifumania nyavu zao kirahisi.

SOMA NA HII  KISA MEYELE KUSEMWA VIBAYA...MANARA ACHARUKA...ATUPA DONGO AZAM NA KWA MSEMAJE WAO....

Uwezo wa Makambo na Mayele katika kufumania nyavu unategemewa kuwa kipimo kwa Varane pamoja na Ouattara ambao ni mahiri katika kudhibiti washambuliaji wa timu pinzani wameanza kufanya hivyo kwenye mchezo dhidi ya St George.

Mayele kwenye mchezo wa ngao msimu uliopita aliibuka shujaa baada ya kuwafungia bao Yanga amblo ndio liliamua ubingwa wa Ngao ya Jamii, Ki aliwafunga Simba kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa akiwa na Asec Mimosas kabla hajatua Yanga huku Morrison pia hakuwaweza Simba misimu miwili iliyopita kwenye ngao.

Pembeni, Mohamed Hussein na Kapombe watakuwa na kibarua cha kukabiliana na mawinga wenye kasi, Morrison na Ki.

Morrison na Ki mbali na kasi, wana uwezo mkubwa wa kupiga krosi na chenga wanakutana na mabeki wenye uzoefu mkubwa na ligi sambamba na mashindano ya ndani hivyo tunatarajia ushindani wa kutosha kutoka kwenye nafasi hizo.

Wakati hali ikitarajiwa kuwa hivyo upande wa Simba, mabeki wanne wa Yanga Djuma Shaban, Joyce Lomalisa, Bakari Mwamnyeto na Yannick Bangala nao hawatokuwa na shughuli nyepesi kutoka kwa mastraika wa watani wao Moses Phiri, Pape Sakho, Habib Kyombo na Nelson Okwa.

Uwezo mkubwa wa kufumania nyavu wa Kyombo na Phiri unawalazimisha mabeki wawili wa kati wa Yanga, Mwamnyeto na Bangala kujiandaa vilivyo ili kuwadhibiti wawili hao.

Msimu uliomalizika, Kyombo ambaye amesajiliwa dirisha hili kubwa la uhamisho akitokea Mbeya Kwanza ameonekana kuzungumzwa zaidi na kocha kuwa ni mchezaji mzuri atasaidiana na Phiri aliyetoka Zanaco ambako alipachika mabao 14.

Wakati upande wa pembeni Lomalisa na Djuma Shaban pia watatakiwa kufanya mazoezi ya pumzi kutokana na kukutana na wachezaji wenye kasi ambao wameonyesha ubora Okwa aliyesajiliwa kutokea Rivers United na mfungaji wa bao bora Afrika Sakho.