Klabu ya Yanga imesema haina mpango wa kumsajili Mshambuliaji wa Vipers United ambaye ni raia wa Congo DR kwani tayari timu hiyo inajitosheleza kwa sasa na hawana mpango wa kusajili mchezaji mwingine.
Hayo yamesemwa na Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Mohammed Nabi na msaidizi wake, Cedric Kaze wakati wakizungumza na wanahabari jana Jumamosi, Agosti 19, 2022 katika dimba la Sheikh Amri Abeid, Arusha baada ya kumalizika mchezo wao na Coastal Union ambapo Yanga waliibuka na ushindi wa bao 2-0.
Baada ya kuulizwa swali iwapo anataka kumsajili Manzoki na iwapo yupo kwenye mipango yake, Nabi alianza kwa kushangaa kwanza kisha akasema;
“Mimi sio kocha wa Simba, mimi ni kocha wa Yanga… Manzoki Yanga? Hapana. Kwa Yanga hakuna kitu chochote kuhusu Cesar Manzoki, sisi tuna wachezaji mastraika wameenea, wachezaji wageni tayari wametosha, hizo habari sio za kweli. Sisi hatumhitaji, kama kuna timu unamhitaju ni wao ila sio Yanga, sisi tunajitosheleza,” amesema Nabi na kocha wake msaidizi Kaze.
Ikumbukwe kuwa, hivi karibuni ziliibuka tetesi kuwa Yanga wametuma ofa kwa Vipers kumtaka Manzoki baada ya Klabu ya Simba kushindwa kumsaini kutokana na changamoto ya kimkataba waliokutana nayo kwa mchezaji huyo.