Home Geita Gold FC A-Z MPOLE AFUNGUKA DILI LAKE NA SIMBA LILIVYOBUMA…AGUSIA TIMU ZA NNJE ZILIVYOMTAKA...

A-Z MPOLE AFUNGUKA DILI LAKE NA SIMBA LILIVYOBUMA…AGUSIA TIMU ZA NNJE ZILIVYOMTAKA NA KUMPOTEZEA….


Bado mashabiki wa soka na hasa wale wa Simba wanajiuliza imekuwaje timu hiyo imemkosa George Mpole, wakati inaelezwa alishapewa mkataba kabisa wa awali ili atue Msimbazi?

Kadhalika wanajiuliza zile tetesi aliikataa Simba ili atimkie nje ya nchi ziliishia wapi, hasa baada ya kushuhudia utambulisho wa kikosi kipya cha timu hiyo kikiwa hakina jina la Mpole.

Gazeti la michezo la Mwanaspoti limefanya jitihada za kumtafuta straika huyo wa Geita Gold na aliyekuwa Mfungaji Bora wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita na kufanya naye mahojiano maalum na mchezaji huyo amefunguka mambo kadhaa ikiwemo kufichua dili lake la Simba lilivyoishia hewani.

Mpole pia anaweka bayana namna Fiston Mayele wa Yanga alivyompa presha kubwa kwenye mbio za kuwania ufungaji bora kwa msimu uliopita. Ebu endelea naye…!

MAISHA BAADA YA TUZO

Anasema baada ya kuchukua kiatu cha dhahabu cha Ligi Kuu Bara, milango ya kiuchumi ya maisha yake imefunguka.

Tayari zipo kampuni zilizomfuata kufanya naye matangazo na anaeleza atasaini muda wowote timu itakaporejea Geita, kwani amefanya nao mazungumzo na amekubaliana nao.

“Umaarufu una faida kuliko changamoto, kama kupata matangazo yatakayoniingizia pesa, nje na hapo umefungua njia ya kuwasiliana na watu mbalimbali ambao ninaweza kufanya nao vitu mbalimbali,” anasema na kuongeza;

“Pia naisaidia familia yangu, na somesha wadogo zangu, namtunza mama yangu mzazi maana baba yangu alifariki dunia nikiwa mdogo tangu mwaka 2005 nikiwa darasa la saba, ndio maana katika kazi ya mpira sitaki kuyumbishwa, mimi naishi kwa uhalisi kwani ninachokifanya na kusema namanisha.”

MAPOKEZI YALIYEYUKA

Viongozi wa Chama Cha Soka Mkoa wa Mbeya (MREFA), kilitaka kumwandalia mapokezi baada ya kuchukua kiatu lakini mambo yakaenda ndivyo sivyo, analifafanua hilo.

“Nilipigiwa simu na viongozi wa Mkoa wa Mbeya ili niseme ratiba zangu waniandalie mapokezi, lakini kipindi hicho nilikuwa kambini na timu ya taifa ‘Taifa Stars’, hivyo nikashindwa kutimiza hilo, pamoja na hayo yote bado wameniambia nikipata muda watanifanyia sherehe, hivyo hilo litafanyika,” anasema.

Anawaambia mashabiki wa mkoa huo (Mbeya ) hali halisi alishindwa kujigawa na hakupata muda wa kwenda kwa kipindi hicho, tofauti na maneno ya watu mtandaoni.

PRESHA KWA MAYELE

Anajikumbusha ya msimu uliopita, bato lake lilivyokuwa baina yake na Fiston Mayele wa Yanga haikumpa presha, aliamini kipaji chake na kufanya kazi inayomhusu, bila kuangalia mpinzani wake anafanya nini.

“Mayele ni mshambuliaji kiongozi katika timu yake na alifanya majukumu yake kikamilifu, hilo halikunifanya niwe na presha, bali nilizingatia nilichokuwa naelekezwa na kocha wangu Fedy Felix ‘Minziro’ na nilikifanya, pia huwa naamini sana kipaji changu na ndiyo maana sipendi kuyumbishwa,” anasema.

Tayari Mayele katupia msimu huu mechi yake ya kwanza Yanga ilipocheza dhidi ya Polisi Tanzania na juzi Jumamosi dhidi ya Coastal Union, kuhusu hilo Mpole anasema; “Akipata nafasi ya kufunga afunge sana, maana hata mimi nikipata nitafunga sana.”

Anasisitiza hana presha kabisa na mwanzo wa Mayele akilinganisha na msimu uliopita hakufunga mechi ya kwanza na ya pili, baada ya hapo alikiwasha.

DILI LA SIMBA

Anakiri alifanya mazungumzo na Simba ila hakukubaliana na baadhi ya vipengele vilivyokuwepo kwenye mkataba na wakati huo huo alipokea ofa mbalimbali kutoka timu za nje.

Kuna taarifa za Mpole amekuwa akizurura na mkataba wa Simba wakati hakukubaliana na ofa yao, anasema; “Sikuwahi kuzurura na mkataba wa Simba baada ya kufanya nao mazungumzo nikaona yapo mambo ambayo sijaridhika nao nikaendelea na maisha mengine. Kifupi Simba ndio waliozingua na sisi mimi.”

Kuhusu dili za timu za nje anasema katika vipengele vya mikataba yao vilihitaji mchezaji mzoefu na michuano ya CAF na yeye hakukidhi masharti yao.

Anaulizwa sasa imekuaje ukashindwa kujiunga na Simba inayoshiriki michuano ya CAF? Anaeleza.

“Mkataba huo ulitakiwa nisaini nikacheze na sio nisubiri nicheze Simba ndio nisaini, ndio maana dakika za mwisho nikaona bora nisalie Geita Gold ambao kila nilichokuwa nakifanya kuanzia hatua ya kwanza hadi hapa nilipofika walijua, ndio maana nipo nao.”

Anaongeza alifuatwa na timu mbalimbali za Ligi Kuu, ambazo kwa wakati huo hakukubaliana na ofa zao.

FAMILIA YA WANASOKA

Anasema ametokea familia ya soka baba yake marehemu, alikuwa anacheza winga mshambuliaji katika timu za mashirika na ndiye aliyemvutia kucheza.

SOMA NA HII  WAKATI STARS IKITUPA KARATA LEO AFCON....HUYU HAPA MCHEZAJI ALIYEITWA KIUPENDELEO...

“Aliyefanya nipende soka ni baba yangu, kwani wakati nikiwa mdogo nilikuwa nakwenda naye Uwanja wa Sokoine Mbeya kuona wanavyocheza, nikitoka hapo anaanza kunifundisha, hivyo sijakurupuka kuingia kwenye soka,” anasema.

“Mimi ni kijana wa kwanza kati ya watoto watano, wote ni wa kiume, wadogo zangu wengine wanacheza viungo washambuliaji, washambuliaji, lakini binafsi sitaki wajikite huko nataka kwanza wasome, mengine watayakuta baadae, elimu ni muhimu sana ndio maana sitaki kuwataja majina.”

AMEBUKUA KINOMA

Kama kuna mashabiki wanamchukulia poa Mpole basi itakuwa imekula kwao, kwani ana degree (Shahada) ya biashara aliyoipata chuo cha SUA kilichopo mkoa wa Morogoro.

“Nina taaluma ya biashara, nilimaliza chuo cha SUA mwaka 2010, najua ninachokifanya katika maisha yangu, tofauti na wanavyonichukulia mashabiki, naona mengi wanavyoongea mitandaoni ila ndiyo maisha siyo kila jambo la kujibu,” anasema.

KIATU NA DUA ZA MAMA

Anasema mama yake Magreth Kasenga ni mwanamaombi, alikuwa anamuombea kila alipokuwa anacheza mechi na alimwambia anaamini atafika mbali.

“Nimezaliwa kwenye familia ya maombi haswa, mama alikuwa anakesha kwa maombi, nakumbuka mechi yangu ya mwisho aliniambia nalala sitaki kuangalia, nitaambiwa na majirani kama umefanikiwa kuibuka kinara ama kachukua mwenzako,” anasema na kuongeza,”

“Siku ya tuzo pia hakuangalia baada ya kumaliza nikampigia, alilia sana, maana mimi namtunza hivyo anajisikia faraja na anaona nimempokea majukumu ya kusomesha wadogo zangu.”

Ukitaka kujua mtoto wa nyoka ni nyoka, basi hilo analithibitisha Mpole ambaye anawaambia Watanzania ni mwanamaombi mzuri kutokana na misingi aliyolelewa na mama yake Magreth.

“ Kitu ambacho hawakijui wengi mimi naomba sana, hakuna kitu nakifanya bila kumtanguliza Mungu, najua kwenye soka kuna ushirikina mwingi ila siamini kama unazidi nguvu za Mungu,” anasema.

AZIOGA NOTI ZA WACHAMBUZI

Mpole anasema wachambuzi wa soka nchini, walimpatia zawadi ya Sh1 milioni kama motisha ya kufanya vizuri, jambo lililomshangaza.

“ Nashukuru sana wachambuzi walionyesha kuna maisha nje ya kazi, maana hawakutaka maisha yetu yaishie uwanjani, hilo limenifunza kujua ushirikiano wetu na wanahabari,” anasema.

KIATU CHA LAKI NA NUSU

Staa huyo ambaye amekuwa akizungumzwa sana midomoni mwa watu kutokana na kile alichokifanya kwenye ligi msimu uliopita ameweka wazi kiatu chake cha kwanza cha soka alinunua elfu 30.

“Nakumbuka nilinunua elfu 30 lakini kwa sasa navaa kiatu kuanzia laki moja na kuendelea, nina viatu vingi sikumbuki idadi lakini kiatu cha kwanza kabisa nilinunua bei hiyo,” anasema na kuongeza;

“Sio kila kiatu ninachovaa nanunua mwenyewe vingine napewa zawadi na mashabiki, najivunia kuwa karibu na watu wanaopenda kazi ninayofanya kwani nanufaika nao kwa namna moja au nyingine.”

Mpole anasema kuna mashabiki wa aina nyingi na kuwafafanua kuna wanaompenda mchezaji nyakati zote na wale wanasubiri matokeo na kile anakichofanya uwanjani.

“Nimekuwa na bahati ya kukubalika na mashabiki japo kuna wengine wanasubiri nifanye vizuri wanisifie na wengine wanasubiri nikosee wanipe maneno makali ya kuniumiza wote nawachukulia kama changamoto sijawahi kujibizana nao naangalia kazi yangu zaidi,” anasema.

MKALI WA NDONDO

Wachezaji wengi wa soka wanaofanya vyema kwenye ligi kipindi cha mapumziko wamekuwa wakitumia muda wao mwingi kwenye mapumziko kucheza mechi za mtaani hilo limethibitishwa na kinara wa mabao msimu uliopita.

“Nimekuwa muumini mkubwa wa kucheza ndondo nacheza sana hadi sasa nikiwa mapumziko huwa natumia muda wangu mwingi kucheza mechi hizo ambazo naamini zinaendeleza uimara wangu,” anasema na kuongeza;

“Huku kwenye ndondo kuna matukio mengi ya kutisha nimeshawahi kushuhudia matukio mengi ya imani za kishirikina kuna kufukua makaburi, kufukia paka ili kuashiria ushindi kwa timu,”

Mpole anasema kuhusu imani za kishirikina hana imani na hivyo vitu na hajawahi kujihusisha navyo anamini katika kipaji na mazoezi huku akikiri kuwa kama ushirikina una nafasi kwenye soka basi wachezaji wenye imani hizo wangekuwa mbali sana.

MUME WA MTU

Mpole ni mume wa mke mmoja waliobahatika kupata mtoto anayeitwa Thiago, lililotokana na kumpenda staa wa Brazil na klabu ya Chelsea inayoshiriki Ligi Kuu ya England, Thiago Silva.

“Natamani mtoto wangu aje kuwa mchezaji na nampenda sana huyo mchezaji ambaye nimempa jina lake, namfuatilia sana kila anapocheza. Pia namkubali sana mshambuliaji, Cristiano Ronaldo wa Manchester United,” anasema.