Home Habari za michezo KISA MAKOSA YA KIZEMBE KWA MABEKI SIMBA…KOCHA MAKI ‘AFURA KWA MANENO’…AWATAJA ONYANGO...

KISA MAKOSA YA KIZEMBE KWA MABEKI SIMBA…KOCHA MAKI ‘AFURA KWA MANENO’…AWATAJA ONYANGO NA INONGA…


Licha ya safu yake ya ulinzi kutoruhusu bao hadi sasa kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu, Kocha Mkuu wa Simba, Mserbia Zoran Maki, amesema bado hajaridhishwa na muunganiko wa timu yake kwa ujumla ikiwamo mabeki.

Simba ambayo iko nchini Sudan kwa mwaliko maalum kutoka kwa Klabu ya Al Hilal, kwa ajili ya kucheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya wenyeji wao hao na Asante Kotoko ya Ghana, ni timu pekee katika Ligi Kuu Bara ambayo hadi sasa haijaruhusu nyavu zake kutikiswa kwenye ligi hiyo.

Katika mechi hizo za Ligi Kuu, Simba ilishinda mabao 3-0 dhidi ya Geita Gold FC, na 2-0 dhidi ya Kagera Sugar, mechi zote zikipigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam huku safu ya ulinzi ikiwa chini ya Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Henock Inonga na Mohamed Quattara.

Hata hivyo, katika safari hiyo ya Sudan licha ya Zoran kupania kwenda kuzitumia mechi hizo kusuka safu yake ya ulinzi, atawakosa Manula, Kapombe, Tshabalala pamoja na kipa namba mbili, Ben Kakolanya kutokana na kubaki nchini kwa majukumu ya timu ya Taifa, Taifa Stars.

Zoran alisema Inonga na Joash Onyango tayari walishakuwa na muunganiko mzuri, hivyo anachokifanya kwa sasa ni kutengeneza kombinesheni nyingine katika safu hiyo kwa kumpa nafasi kubwa Quattara ambaye ameonekana kuwa mtulivu kwenye mechi mbili za ligi ambazo wamecheza.

Alisema hajapata muunganiko mzuri katika kila nafasi, hivyo atahakikisha kila safu inakuwa imara na kumpa nafasi kila mchezaji kwa ajili ya kupata kombinesheni nzuri.

Kocha huyo alisema, katika safu ya ulinzi licha ya kutopoteza mechi wala kuruhusu bao, lakini bado ana kazi kubwa ya kuifanya safu hiyo kuwa imara zaidi na wapinzani kutopita kirahisi.

“Timu inapata matokeo mazuri, lakini bado tuna kazi kubwa ya kuhakikisha tunakuwa imara zaidi kwa kila idara kuwa na muunganiko mzuri,” alisema Zoran.

Simba ambayo inajiandaa kuivaa Nyasa Bigi Bullets ya Malawi kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Septemba 9-11, kabla ya mchezo huo inakabiliwa na mechi ya Ligi Kuu dhidi ya KMC FC Septemba 7, mwaka huu katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.

SOMA NA HII  IMEISHA HIYO....KOCHA MPYA SIMBA KUANZA KAZI NA WACHEZAJI HAWA WANNE..

Ikiwa Sudan, itaanza kushuka dimbani Jumapili wiki hii dhidi ya Asante Kotoko, kabla ya kuhitimisha Agosti 31, mwaka huu kwa kucheza dhidi ya Al Hilal.

Baada ya mechi hiyo, itakwea pipa kurejea Dar es Salaam tayari kwa mechi nyingine ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya AS Arta Solar 7 ya Djibouti inayoundwa na baadhi ya nyota wakubwa waliowahi kucheza klabu kubwa Ulaya, Kiungo Mcameroon Alex Song na winga Solomon Kalou raia wa Ivory Coast.

Song, aliwahi kuichezea Klabu ya Arsenal ya England na Barcelona ya Hispania, wakati Kalou anakumbukwa kwa kazi kubwa aliyoifanya Chelsea wakati akiitumikia.