Home Habari za michezo SUALA LA MANZOKI KUTUA SIMBA NI MUDA TU UNANGOJEWA….AFUNGUKA A-Z UKWELI WA...

SUALA LA MANZOKI KUTUA SIMBA NI MUDA TU UNANGOJEWA….AFUNGUKA A-Z UKWELI WA MKATABA WAKE NA VIPERS…


Mshambuliaji wa Vipers ya Uganda, Cesar Lobi Manzoki amevunja ukimya na kuweka bayana ni suala la muda tu kwake kuja kucheza Simba msimu huu, huku akikanusha kuwa na mkataba wa miaka miwili na klabu hiyo ya Uganda aliyokuja nao juzi kuvaana na Yanga.

Manzoki alisema ni kweli ana mkataba na Vipers lakini hauzidi miezi mitatu na hizo taarifa kwamba ni wa miaka miwili ni udanganyifu ambao tayari menejimenti yake imeanza kulishughulikia na asingependa kulizungumza kwa undani zaidi.

Manzoki alisema klabu ya Vipers inajua mkataba baina yao umebaki wa muda gani na kama wataendelea kushikilia hilo la miaka miwili kuwa eti atamaliza kuitumikia Vipers 2025, hatakwenda mazoezini, katika mechi wala shughuli yoyote ya timu hiyo.

“Muda niliokwambia umebaki kwenye mkataba wangu ndio sahihi, hilo jingine wala silifahamu na naamini baada ya kufikia ukingoni nitaondoka hapa Vipers kwenda katika timu nyingine,” alisema Manzoki na kuongeza;

“Nitakuja kucheza hapa Tanzania na klabu yangu mpya itakuwa Simba, hilo si suala la kuficha tena kutokana na kitu ambacho wamekifanya Vipers wala sijapendezewa nacho na si vizuri.”

Manzoki aliyeiwezesha Vipers kubeba ubingwa wa Uganda msimu uliopita, alifafanua; “Wakala wangu yupo katika mazungumzo mazuri na viongozi wa Simba na kilichokuwa kimekwamisha ni hiyo miezi michache iliyobaki katika mkataba wangu na si kama wao walivyoeleza si jambo la kweli.

“Vipers wenyewe wanaelewa hilo walilofanya ni kosa kwani mkataba wao na ule uliopo kwenye mtandao ni tofauti. Siwezi kuhitajika na timu kubwa kama Simba na nikakataa kwenda.”

Alifichua pia tayari kuna hatua mbili kubwa zimefanyika kwa upande wake ameandika barua Shirikisho la Soka la Uganda (FUFA) na lile la kimataifa (FIFA) ili kulalamikia kubambikiwa mkataba usio halali.

“Nikiwa nasubiri majibu huko, Simba nao tayari wameandika barua kwenda Vipers kuhusu kuhitaji huduma yangu kwa maana hiyo nina imani kubwa nitakuja kucheza hapa msimu huu na nitaingia kwenye ule usajili wa dirisha dogo kwani huu wa sasa utakuwa umefungwa.”

SOMA NA HII  WAKATI AKIZINGUA MAN UTD....RONALDO AKAMILISHA UJENZI WA HOTEL LA KIFARAHI MOROCCO...

Kocha wa Vipers, Roberto Oliveira alisema anatamani sana kumuona Manzoki ambaye alikuwa ni mfungaji bora wa Ligi ya Uganda kwa msimu uliopita akiendelea kusalia Vipers.

“Mimi nimeongea na Manzoki nakumwambia shauku yangu, ni mchezaji wangu bora na natamani kuwa naye msimu hadi msimu, lakini kwenye hili wanaokuwa na uamuzi wa mwisho ni viongozi,”

“Naelewa yeye kama mchezaji ana malengo yake, mimi pia nina malengo yangu kwahiyo nimewasilisha maombi kwa mabosi wa timu kuona kama watakubali kumbakisha,” alisema Oliveira aliyethibitisha amewahi kuongea na mchezaji ili kuona kama atakubali kubaki na kuongeza mkataba.