Home Habari za michezo UWEPO WA TSHISHIMBI NA CHIRWA WAMPA KIBURI KATWILA NA IHEFU YAKE…AOMBA LIGI...

UWEPO WA TSHISHIMBI NA CHIRWA WAMPA KIBURI KATWILA NA IHEFU YAKE…AOMBA LIGI IANZE USIKU HUU…


Kocha Mkuu wa Ihefu, Zuberi Katwila ameangalia uwezo wa nyota wake akiwamo kiungo, Papy Tshishimbi na kutamka wazi kuwa vijana wake wameiva na wapo tayari kwa Ligi akibainisha kuwa mapungufu ni madogo sana yaliyobaki.

Ihefu katika usajili wake inajivunia nyota wenye majina makubwa waliowahi kutamba na timu kubwa za Simba, Yanga na Azam wakiwamo Tshishimbi, Nicolas Wadada, Never Tigere na Obrey Chirwa.

Akizungumza baada ya mchezo wao dhidi ya Ken Gold kwenye michuano ya Samia Pre Season Cup waliposhinda penalti 5-4 na kutinga fainali, Katwila alisema nyota wake wameiva na sasa wanasubiri Ligi ianze waingie uwanjani rasmi.

Alisema wachezaji wote wameonesha kiwango bora na cha kumvutia huku akiwataja baadhi yao, akiwamo Tshishimbi kuwa anatarajia makubwa kuanzia Agosti 15 watakapoanza Ligi kwa kuwakaribisha Ruvu Shooting.

“Kwa ujumla wameiva, kilichobaki ni kutafuta kombinesheni ya kujua nani acheze na nani ila hadi sasa tuko tayari kwa Ligi Kuu na vijana wanaonesha ubora wao na nia ya kuisaidia timu,” alisema Katwila.

Kocha huyo aliongeza pamoja na kuridhishwa na kiwango cha wachezaji lakini bado sehemu ya ufungaji mabao ina mapungufu madogo, akibainisha kuwa utimamu wa mwili uko sawa.

Kwa upande wake mchambuzi wa soka jijini hapa, Yusuph James alisema katika mechi za kirafiki walizocheza Ihefu, lazima nao wajitathimini kwani matokeo yao hayakuwa ya kulingana na ubora wa kikosi tofauti na walivyotarajia.

“Kwenye michuano hii, walishinda 1-0 dhidi ya U20 ya Mbeya City, wakashinda idadi hiyo tena na Kombaini ya Kyela DC na penalti 5-4 na Ken Gold baada ya suluhu ya bila kufungana lazima hapo waone kwama kuna tatizo eneo la ushambuliaji benchi la ufundi lishtuke mapema,” alisema James.

SOMA NA HII  KUELEKEA 'KARIKAOO DERBY'...BENCHIKHA AWAPA KISOMO MASTAA WOTE SIMBA...