Home Habari za michezo WAKATI AKIJUA LAZIMA ATAKUTAA NA YANGA…IBENGE AFUNGUKA HAYA KUHUSU SIMBA NA UWEPO...

WAKATI AKIJUA LAZIMA ATAKUTAA NA YANGA…IBENGE AFUNGUKA HAYA KUHUSU SIMBA NA UWEPO WAO SUDAN….


Kocha Mkuu wa Al Hilal Omdurman ya Sudan Florent Ibenge amesema ushiriki wa Simba SC katika michuano maalum iliyoandaliwa na Klabu hiyo, itakisaidia sana kikosi chake kinachojiandaa na Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.

Ibenge ametoa kauli hiyo baada ya Al Hilal kuanza vyema michuano hiyo kwa kuifunga Asente Kotoko 2-0, katika mchezo uliounguruma Uwanja wa Al Hilal.

Kocha huyo kutoka DR Congo amesema anaifahamu vizuri Simba SC, kutokana na kuwa na kikosi bora ambacho kwa miaka ya hivi karibuni, kimefanya vizuri kwenye Michuano ya Kimataifa inayoratibiwa na Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’.

Amesema ushiriki wa Simba SC kutoka Tanzania kwenye michuano hiyo, una manufaa makubwa sana kwake na kwa wachezaji wa Al Hilal, hivyo wataipa heshima zote klabu hiyo watakapocheza nayo Jumapili (Agosti 28) katika Uwanja wa Al Hilal.

“Mchezo dhidi ya Simba SC utakuwa na manufaa sana kwetu, Simba SC ni timu yenye uzoefu. Mchezo huu utatuletea mambo hasi na chanya tunayohitaji katika maandalizi yetu. Tunahitaji michezo hii kabla ya kampeni yetu ya Ligi ya Mabingwa Afrika.” amesema Ibenge

Kocha Ibenge amekutana na Simba SC mara sita akiwa na klabu za AS Vita ya nchini kwao DR Congo na RS Berkane ya Morocco, akishinda michezo miwili, akipoteza michezo minne.

Akiwa na AS Vita msimu wa 2018/19, Ibenge aliifunga Simba SC mabao 5-0 Hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika mjini Kinshasa (DR Congo), Mchezo wa Mzunguuko wa pili msimu huo ukichezwa Dar es salaam Ibenge na AS Vita yake alikubali kulala 2-1 Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Msimu wa 2020/21 akiwa na AS Vita Ibenge alikubali kufungwa na Simba SC mjini Kinshasa 1-0 hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, Mchezo wa Mzunguuko wa pili msimu huo alipoteza tena jijini Dar es salaam kwa kufungwa 4-1 Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Msimu wa 2021/22, Ibenge akiwa na RS Berkane aliifunga Simba SC 2-0 mjini Berkane (Morocco) Hatua ya Makundi Kombe la Shirikisho Barani Afrika, Mchezo wa Mzunguuko wa pili msimu huo alikubali kufungwa 1-0, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

SOMA NA HII  KAMWAGA AKATAA KUONGEZA MKATABA SIMBA...AMTAJA MO DEWJI..

Katika mchezo wa Michuano maalum iliyoandaliwa na Klabu ya Al Hilal ya Sudan, Wenyeji walipata ushindi dhidi ya Asante Kotoko ya Ghana, mabao yakifungwa na Lamin Garjo na Khaki Wad wote raia wa Sudan.

Al Hilal ni mojawapo ya Klabu ambazo huenda zikakutana na Young Africans ya Tanzania kwenye Michuano ya Ligia ya Mabingwa Barani Afrika, hatua ya kwanza.

Mshindi wa mchezo wa Young Afrika dhidi ya Zalan FC ya Sudan Kusini atacheza na mshindi wa mchezo wa Al Hilal dhidi ya St George ya Ethiopia.

Kabla ya kutua Al Hilal Ibenge alikua Kocha Mkuu wa RS Berkane ya Morocco, akiiwezesha klabu hiyo kutwaa Ubingwa wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika kwa kuifunga Orlando Pirates ya Afrika Kusini.