Home Habari za michezo WAKATI ONYANGO AKISEMEKANA KUTOKUWA NA FURAHA SIMBA….KOCHA MAKI AIBUKA NA HILI JIPYA...

WAKATI ONYANGO AKISEMEKANA KUTOKUWA NA FURAHA SIMBA….KOCHA MAKI AIBUKA NA HILI JIPYA LINALOMUHUSU…


Kocha Mkuu wa Simba SC, Mserbia Zoran Maki amemjibu beki wa Kimataifa kutoka nchini Kenya Joash Onyango ambaye anatajwa kuwa kwenye mpango wa kuwasilisha maombi ya uvunjwa kwa mkataba wake.

Onyango anatajwa kuwa mbioni kufanya hivyo, kufuatia kutoridhishwa na maamuzi ya Kocha huyo raia Serbia, kumuweka Benchi na kuwatumia Mabeki Henock Inonga na Mohamed Ouattara katika michezo miwili ya Ligi Kuu Tanzania Bara waliyocheza hadi sasa.

Katika michezo hiyo, Simba ilishinda mabao 3-0 dhidi ya Geita Gold FC, na 2-0 dhidi ya Kagera Sugar, mechi zote zikipigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam huku safu ya ulinzi ikiwa chini ya Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Henock Inonga na Mohamed Ouattara.

Zoran amesema Inonga na Joash Onyango tayari walishakuwa na muunganiko mzuri, hivyo anachokifanya kwa sasa ni kutengeneza kombinesheni nyingine katika safu hiyo kwa kumpa nafasi kubwa Ouattara ambaye ameonekana kuwa mtulivu kwenye michezo aliyocheza.

Amesema hajapata muunganiko mzuri katika kila nafasi, hivyo atahakikisha kila safu inakuwa imara na kumpa nafasi kila mchezaji kwa ajili ya kupata kombinesheni nzuri.

Kocha huyo ameema, katika safu ya ulinzi licha ya kutopoteza mchezo wala kuruhusu bao, lakini bado ana kazi kubwa ya kuifanya safu hiyo kuwa imara zaidi na wapinzani kutopita kirahisi.

“Timu inapata matokeo mazuri, lakini bado tuna kazi kubwa ya kuhakikisha tunakuwa imara zaidi kwa kila idara kuwa na muunganiko mzuri,” amesema Zoran.

Simba ambayo inajiandaa kuivaa Nyasa Bigi Bullets ya Malawi kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Septemba 9-11, kabla ya mchezo huo inakabiliwa na mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya KMC FC Septemba 7, mwaka huu katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Katika kujiandaa na michezo hiyo itakayochezwa mwezi ujao, Simba SC itacheza michezo wa Kimataifa wa Kirafiki katika Michuano maalum iliyoandaliwa mjini Omdurman-Sudan na klabu ya Al Hilal.

Katika safari ya kuelekea Sudan Zoran atawakosa Manula, Kapombe, Tshabalala pamoja na kipa namba mbili, Ben Kakolanya kutokana na kubaki nchini kwa majukumu ya timu ya Taifa, Taifa Stars.

SOMA NA HII  NIYONZIMA- RWANDA NA YANGA NI DAMU DAMU....

Ikiwa Sudan, itaanza kushuka dimbani Jumapili wiki hii dhidi ya Asante Kotoko, kabla ya kuhitimisha Agosti 31, mwaka huu kwa kucheza dhidi ya Al Hilal.

Baada ya mechi hiyo, itakwea pipa kurejea Dar es Salaam tayari kwa mechi nyingine ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya AS Arta Solar 7 ya Djibouti inayoundwa na baadhi ya nyota wakubwa waliowahi kucheza klabu kubwa Ulaya, Kiungo Mcameroon Alex Song na winga Solomon Kalou raia wa Ivory Coast.

Song, aliwahi kuichezea Klabu ya Arsenal ya England na Barcelona ya Hispania, wakati Kalou anakumbukwa kwa kazi kubwa aliyoifanya Chelsea wakati akiitumikia.