Kocha Mkuu wa Simba SC Zoran Maki amemwagia sifa kedekede Kiungo Mshambuliaji wa kikosi chake Clatous Chotta Chama kwa kusema ni mchezaji wa Daraja la juu.
Chama aliyerejea Simba SC wakati wa Dirisha Dogo la usajili mapema mwaka huu akitokea RS Berkane alikouzwa mwanzoni mwa msimu uliopita, amekuwa na kiwango bora tangu kuanza kwa msimu huu 2022/23.
Zoran amesema kiungo huyo kutoka Zambia amekua na kiwango bora ambacho kinaisaidia timu inaposhambulia, hivyo anafarijika kuwa na mchezaji kama huyo mwenye utulivu akiwa na mpira na kutoa pasi za uhakika.
Amesema Chama anaweza kutengeza nafasi za kufunga na amefanya hivyo katika Michezo ya Ligi Kuu hadi Michezo ya Kimtaifa ya Kirafiki na uzuri anafunga mwenyewe muda mwingine kulingana na shambulizi lilivyo.
“Ninahitaji kuona Chama anafanya hivi si katika Michuano ya ndani, bali ninataka kuona akiendelea kuwajibika hadi kwenye Michuano ya Kimataifa, akifanya hivyo basi atakua ni sehemu ya silaha zangu kubwa katika kufikia malengo yetu Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.” amesema Zoran Maki.
Hadi sasa Chama amefunga bao moja katika Mshike Mshike wa Ligi Kuu Tanzania Bara na kusababisha mabao kadhaa yaliyoipa ushindi Simba SC katika Michezo ya ligi hiyo.
Pia alionyesha uwazo mkubwa kwenye Michuano maalum nchini Sudan, akifunga bao moja katika ushindi wa 4-2 dhidi ya Asante Kotoko ya Ghana.