Home Azam FC UNAAMBIWA HUYU KOCHA MPYA WA AZAM FC NI MZEE WA MAKOMBE TUU….AL...

UNAAMBIWA HUYU KOCHA MPYA WA AZAM FC NI MZEE WA MAKOMBE TUU….AL AHLY YA MISRI WANAIJUA ‘SHOW’ YAKE…


Hatimaye Uongozi wa Azam FC umekamilisha mchakato wa kumpata Kocha Mkuu, baada ya kuvunja mkataba wa Kocha kutoka nchini Marekani Abdihamid Moallin mwishoni mwa mwezi Agosti.

Azam FC imethibitisha kukamilisha mchakato wa Kocha huyo kupitia kurasa zake za Mitandao ya kijamii usiku wa kuamkia leo, huku ikielezwa kuwa Kocha huyo anatarajiwa kuwasili nchini Tanzania leo Jumanne (Septembe 06).

Taarifa ya Azam FC iliyochapishwa kwenye kurasa zao za Mitandao ya kijamii inaeleza: Tunayofuraha kuwataarifu kuwa tumefikia makubaliano na Denis Lavagne, kuwa Kocha wetu Mkuu.

Kocha huyo raia wa Ufaransa, mwenye wasifu mkubwa, akiwa na leseni ya juu ya ukocha (UEFA Pro Licence), anakuja kuchukua mikoba ya Abdihamid Moallin.

Lavagne anatarajia kutua nchini leo Jumanne, tayari kuanza rasmi majukumu yake hayo.

Mfaransa huyo, ni kocha wa viwango vya juu sana akiwa na uzoefu na soka la Afrika, amewahi kufundisha timu ya Taifa ya Cameroon (2011-2012), miamba ya Algeria, USM Alger na JS Kabylie.

Aidha amewahi kufundisha vigogo wa Tunisia, Etoile Du Sahel (2013), Smouha ya Misri, Coton Sports (Cameroon), Al Hilal ya Sudan.

Moja ya mafanikio yake ni kufika fainali ya michuano ya Lugi ya Mabingwa Afrika mwaka 2008 akiwa na Coton Sport ya Cameroon na kupoteza dhidi ya Al Ahly ya Misri kwa jumla ya mabao 4-2.

Ubora wa mbinu zake, zilimwezesha mwaka jana, kuiongoza JS Kabylie ya Algeria kushika nafasi ya pili kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, ikicheza fainali na Raja Casablanca ya Morocco na kupoteza kwa mabao 2-1.

Mtaalamu huyo ni kocha wa makombe, kwani aliiwezesha Coton Sport kutwaa mataji manne ya ligi (2007, 2008, 2010, 2011), aliiongoza Al Hilal kutwaa taji la ligi mwaka 2016, aliiongoza JS Kabylie kubeba taji la Kombe la FA (2021) na Etoile Du Sahel kutwaa ubingwa kama huo Tunisia mwaka 2013.

SOMA NA HII  ROBERTINHO ATAMBA KUHUSU KIKOSI CHA SIMBA