Chelsea ilimtimua kocha wao mkuu Mjerumani Thomas Tuchel hapo jana. Huku baada ya akifukuzwa, kuna ripoti kwamba alikataa nafasi mbili za kazi kutoka kwa wababe wa Ulaya msimu uliopita. Tuchel aliamua kutoondoka Stamford Bridge kwenda Barcelona na Manchester United.
Tuchel aliivumilia timu katika mzozo uliosababishwa na vita kati ya Urusi na Ukraine msimu uliopita, ambao ulisababisha timu hiyo kubadilisha umiliki baada ya kuwekewa vikwazo kwa mmiliki wao wa zamani Roman Abramovich. Kipindi hicho hicho pia Chelsea iliwekewa vikwazo vya kifedha na serikali ya Uingereza.
Barcelona walikuwa na nia ya kutaka kumnunua Mjerumani huyo baada ya kumtimua Ronald Koeman kufuatia matokeo mabaya Camp Nou msimu uliopita, lakini Mjerumani huyo alikataa kujiunga na wababe hao wa Uhispania.
Jibu hilo hilo lilitolewa kwa Manchester United, ambao walikuwa wanataka kumsajili meneja huyo wa zamani wa Borussia Dortmund kama mbadala wa meneja wa muda Ralf Rangnick mapema mwaka huu.
Baada ya Chelsea kuanza vibaya msimu huu kwa kushinda mechi tatu tu kati ya saba, na baada ya kupoteza dhidi ya Dinamo Zagreb katika mchezo wa kwanza wa ligi ya mabingwa barani Ulaya. Mmiliki mpya wa Chelsea Todd Boehly akaamua kumfuta kazi Tuchel.