Kocha Mkuu wa kikosi cha timu ya wanawake cha Simba, Simba Queens, Sebastian Nkoma tayari ameshatinga kambi ya Simba iliyopo Lilongwe Malawi ili kuliongezea nguvu benchi la timu hiyo inayojiandaa kuivaana Nyasa Big Bullets ya Malawi katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Nkoma aliondoka asubuhi ya jana kwa usafiri wa shirika la ndege la Malawi na taarifa zilizopatikana ni kwamba tayari ameshatimba kambi ya timu hiyo iliyopo hoteli ya President Waltmont kuungana na Juma Mgunda na Seleman Matola waliotangulia mapema.
Taarifa kutoka ndani ya Simba zinasema kuwa Nkoma ameenda kuwa kama kocha wa viungo tofauti na taarifa ya awali iliyotoka klabuni humo ikieleza aliwahishwa huko ili kuokoa jahazi kutokana na sintofahamu ya kocha Mgunda mwenye kiwango cha elimu ya leseni A ya ukocha, japo ilidaiwa cheti chake kilikuwa hakijatoka.
“Nkoma tayari tupo kambini na sasa tunajiandaa kwenda kwenye mkutano kabla yab mechi (pre match meeting) na hali ya kambi ipo freshi tayari kwa mchezo huo wa kesho {leo} Jumamosi,” kilisema chanzo chetu kilichopo kambi ya Simba.
Taarifa ya kupelekwa kwa Nkoma kwenye kambi ya Simba, imeibuka mijadala kwa wadau wa soka na kusababisha Shirikisho la Soka kutoa orodha ya waamuzi wenye daraja hilo, likiwamo jina la Mgunda .
Katika orodha hiyo, TFF iliainisha makocha 42, akiwamo marehemu Sylvester Marsh aliyefariki dunia mwaka 2015 kabla ya kusahihisha baadaye na kutoa taarifa mpya.
Simba imelazimika kumchukua Mgunda aliyekuwa akiinoa Coastal Union ili kuziba nafasi ya Zoran Maki aliyeachana na klabu hiyo baada ya kupata dili nono klabu ya Al Ittihad ya Misri.