Mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga inaanza kampeni zake kwenye hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kucheza na Zalan FC ya Sudan Kusini.
Yanga inaanzia ugenini kwenye mchezo wa kwanza utakaopigwa kesho katika Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, marudiano kufanyika katika uwanja huo huo, Septemba 17.
Zalan imeamua kutumia Uwanja wa Benjamin Mkapa kwenye mchezo huo kutokana na viwanja vyake nchini Sudan kukosa hadhi ya kuchezea mashindano.
Ilipotokea
Timu hii imetokea katika Mji wa Rumbek, uliopo katikati ya nchi ya Sudan Kusini, huku ikiwa haina umri mrefu tangu ianzishwe, kwani ilianza 1999, tofauti na wapinzani wao kwenye mashindano, Yanga iliyoanzishwa 1935.
Zalan inashiriki kwenye ligi ya Sudan, ambayo kutokana na machafuko ya hapa na pale imekuwa ikisimamiwa chini ya uangalizi wa Serikali.
Mara ya kwanza
Kutokana na msimu bora uliopita, timu hii imepata nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara yake ya kwanza.
Zalan imekuwa ikitumia jezi zenye rangi nyeupe zenye michirizi na maandishi yenye rangi nyekundu na bukta nyekundu inapocheza mechi ya nyumbani, wakati ugenini ikitumia nyeupe zenye ufito wa bluu au nyeupe na bukta nyeusi.
Mafanikio
Msimu uliopita ndiyo mara yao ya kwanza kushinda ubingwa wa Ligi Kuu nchini humo, huku pia ikishinda Kombe la Shirikisho 2018.
Zalan ilimaliza nafasi ya pili kwenye Kundi B, 2017, ilipofungwa na Gonzaga mabao 4-2 kwenye ligi ya Taifa la Sudan (The South Sudan National League (SSNL) mjini Juba, kabla ya kutwaa ubingwa 2018 kwa kuifunga Gold Star mabao 4-0.
Msimu wa kwanza wa ligi hiyo ulikuwa 2013, ikiwa ni mwaka mmoja baada ya Sudani Kusini kutangaza kupata uhuru wake.
Agosti 18 Klabu hiyo ilimtangaza rasmi, Baping Alliab kuwa kocha wao mpya akitokea timu ya Al Hilal Wau ya Sudan Kusini, aliyechukua nafasi ya Richard Ola.
Ikijipima nguvu
Tangu kuteuliwa kwa Baping Alliab, timu hiyo imecheza michezo mitatu ya kirafiki, ikianza na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Gonzaga, mechi iliyopigwa Agosti 23, kisha kushinda 2-1 mbele ya Homeland Agosti 27, kabla ya suluhu na timu ya vijana ya Sudan Kusini (U-23) Septemba 5.
Mshindi wa jumla kati ya Yanga na Zalan atacheza na mshindi kati ya mabingwa wa Ligi Kuu Ethiopia, St George au Al Hilal ya Sudan.