Home Habari za michezo ISHU YA UWEZO WA FEI TOTO NA SIASA ZA ZNZ ZAMFANYA EDO...

ISHU YA UWEZO WA FEI TOTO NA SIASA ZA ZNZ ZAMFANYA EDO KUMWEMBE KUIBUKA NA MADAI HAYA MAZITO…


Edo Kumwembe/MwanaSpoti

Fei Toto akifunga bao, popote anapocheza huwa nasikitika kidogo. Iwe katika jezi ya Yanga ambayo ameifungia mara nyingi, au Taifa Stars ambayo huwa anaifungia mara chache. Inanikumbusha mambo mengi.

Majuzi alifunga bao zuri dhidi ya Zalan ya Sudan Kusini. Fei anafurahia soka. Hachezi soka kwa hasira. Anajua mpira. Anacheza kwa umaridadi mkubwa lakini zaidi anaweza kuwa kiungo mshambuliaji anayefunga zaidi katika Ligi yetu.

Kila anapofunga bao huwa nakumbuka kwamba Fei anaweza kuwa alama pekee kubwa ya soka la Zanzibar katika mpira wetu. Fei ndiye Mzanzibar anayetemba zaidi katika timu kubwa tatu nchini. Simba, Yanga na Azam.

Fei ndiye mchezaji Mzanzibar mwenye uhakika wa namba katika kikosi cha timu ya taifa. Zamani nilikuwepo katika zama ambazo Wazanzibar watatu au wanne walikuwa na uwezo wa kuanza katika kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania. Sio tu kwamba walikuwa wanaitwa, bali walikuwa wanaanza kikosini.

Na sio kwamba walikuwa wanacheza Simba au Yanga, hapana. Walikuwa wanacheza katika timu za kwao. Small Simba, Malindi, Mlandege, KMKM na nyinginezo. Yaani wanatoka katika Ligi Kuu ya Zanzibar na kucheza katika kikosi cha Taifa Stars moja kwa moja.

Walikuwepo kina Ally Bushiri, Seif na Salum Bausi, Nassor Mwinyi Bwana, Seif Nassoro, Amour Aziz, Riffat Said, Ally Sharrif Adolph na wengineo. Kati yao ni Riffat tu ndiye ambaye aliwahi kuja kucheza bara akisaini Yanga.

Vinginevyo wengine hawa walikuwa wanacheza huko huko na walikuwa wanacheza moja kwa moja katika kikosi cha timu ya taifa. Na kwa wakati huo ilikuwa ngumu kweli kweli kuchuana na wachezaji wa Bara ambao walikuwa na vipaji vikubwa kama kina Said Mwamba, Hamis Gaga, Athuman China na wengineo.

Leo sio tu kwamba hawachezi, bali pia hawaitwi. Lakini kama Taifa Stars ni mtihani mgumu bali hata kuja kutamba Simba na Yanga imekuwa mtihani mgumu kwao. Wapo wanaocheza huku lakini viwango vyao sio vya kutamba. Amebakia Fei tu.

Kabla ya Fei, mastaa wa Zanzibar waliokuwa wanatamba katika kikosi cha timu ya taifa walikuwa Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ambaye alikuwa ni nahodha wetu, pamoja na Abdi Kassim ‘Babi’. Kama utamuhesabu Aggrey Morris kuwa mmoja wao basi tunaweza kumuongeza katika kundi.

Katika klabu zetu kubwa wanazidi kupotea. Kwa mfano, Mudathir Mudathir ameondoka zake Azam na si ajabu akaibukia katika timu ndogo. Ina maana kuna Mzanzibar mwingine ameondoka. Hii ni sawa na akina Mohamed Banka, Abdulaziz Makame na wengineo ambao wanaondoka.

Yanga wana Wazanzibar wawili wengine ambao ni walinzi wa kati. Shaibu Ninja pamoja na Ibrahim Bacca. Hata hivyo maji yameonekana kuwa mazito kwake na badala yake wanaoanza mara kwa mara pale ni Bakari Mwamunyeto na Dickson Job.

Hapo hapo kumbuka kwamba kuna Mzanzibar mwingine, Ibrahim Ame ameonekana kuchemsha Simba na sasa yupo KMC. Labda anaweza kurudi tena katika kiwango cha juu lakini ukweli ni kwamba alama pekee ya Zanzibar inayotesa zaidi kwa sasa ni Fei Toto.

SOMA NA HII  SIMBA INAMTU HUYU MMOJA TU

Nini kinatokea Zanzibar? Kuna mahali wamekosea au wanaendelea kukosea. Kwanza kabisa klabu zao zimeshuka, lakini nahisi uwezo wa mchezaji mmoja mmoja pia umeshuka. Vyote viwili vimekwenda chini kwa wakati mmoja.

Kwanini kila kitu kimekwenda chini? Majuzi nilikuwa napiga stori na watu wa Zanzibar nikiwa pale Zanzibar. Ukweli ni kwamba kwa sababu za kitamaduni Zanzibar haijakubali kuingia katika mfumo wa kisasa wa mabadiliko ya mchezo wenyewe.

Wanaoweza kudhamini mchezo wa soka kwa sasa ni wale ambao hawaruhusiwi kwa mujibu wa sheria za kidini. Wanaoweza kudhamini ni kampuni za ubashiri pamoja na kampuni za pombe. Lakini wote hawa hawaruhusiwi kwa mujibu wa imani za kidini Zanzibar. Hauwezi kulaumu kwa sababu kila watu wana uhuru wao wa kuabudu.

Vinginevyo huku bara tunapata faida ya kukaribishwa wadhamini wa aina hii katika nyanja mbalimbali. Kuna timu kama tano za Ligi Kuu ya Tanzania ambazo zinadhaminiwa na kampuni ya ubashiri. Timu yetu kubwa ya Taifa inadhaminiwa na kampuni ya kilevi.

Zamani kulikuwa na uwanja wa haki kwa sababu mambo haya yalikuwa hayajaingia na pia mpira ulikuwa wa ridhaa zaidi. Leo mpira umetawaliwa na pesa katika kila idara na ni ngumu kuepuka jambo hili kwa urahisi.

Pengo kati ya bara na Visiwani litaendelea hivi kwa muda mrefu na ni rahisi tu kulipima. Chukulia michuano ya Kombe la Mapinduzi kama mfano.

Kwa miaka mingi sasa mashabiki wa soka la Zanzibar wamekuwa wakichukulia michuano hii kama ya kutazama ubabe wa Simba, Yanga na Azam katika soka letu.

Mara nyingi timu za Zanzibar zimekuwa zikitolewa katika hatua ya mwanzo kabisa na baada ya hapo Uwanja wa Aman unajaza mashabiki kuendelea kutazama mechi za Simba na Yanga. Zamani kulikuwa na michuano ya kombe la Muungano na ujinga huu ulikuwa hautokei.

Timu za Zanzibar zilikuwa zinapambana hasa na timu za bara. Baadaye zilipambana hadi kunasa wachezaji wazuri kutoka Bara. Edibily Lunyamila, Nico Bambaga na Clement Kahabuka ni miongoni mwa mastaa waliotoka Bara kwenda kucheza Zanzibar wakiwa katika ubora wao. Leo unadhani Jonas Mkude anaweza kwenda kusaini KMKM?

Wakati huo mpira ulikuwa unategemea wafadhili, siku hizi mpira umeanza kutegemea wadhamini. Hapo ndipo Wazanzibar walipoachwa nyuma na soka letu. Wakati mwingine unajiuliza ni mpaka lini Zanzibar itaendelea kumtegemea Fei kama alama yao kubwa katika soka letu?

Rafiki zangu ambao nilikuwa napiga nao stori pale Zanzibar wote walikiri kwamba ni kweli soka lao limepiga hatua nyingi kwenda nyuma na sio kwamba wachezaji wa bara wanapendelewa kama stori zilivyokuwa zinaibuka miaka kadhaa hapo katikati.

Kuna jambo lazima lifanyike Zanzibar. Ukweli ni kwamba vipaji vipo lakini mwendelezo wa vipaji haupo kama zamani.

Kila siku naona vipaji vingi vya watoto Zanzibar wakiwa wamemwagika katika viwanja mbalimbali mida ya mchana.

Najua tu kwamba wanaenda kukwama mahali.