Kipa wa Mtibwa Sugar, Farouk Shikhalo amekiri ameumia timu yake kupoteza mchezo wa kwanza katika Ligi Kuu Bara msimu huu, lakini kati ya mabao matatu aliyotunguliwa, lile la tatu la kiungo mshambuliaji, Stephane Aziz Ki ndilo lililomuumiza zaidi.
Katika mchezo huo wa raundi ya nne uliopigwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Yanga iliibuka na ushindi wa 3-0 mabao yaliyofungwa na Djuma Shaban, Fiston Mayele na Stephane Aziz Ki na kuifanya Mtibwa kupoteza mchezo wake wa kwanza kwa msimu huu.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Shikhalo alisema licha ya ubora wa mabao yote ila Aziz Ki alitumia akili kufunga bao lake.
“Niliumia kwa sababu wakati anapiga ule mpira tulikuwa wengi golini, unaweza sema ni uzembe wetu lakini huwezi kusita kumpa pongezi mpigaji kwani alitumia udhaifu wetu kutuadhibu hivyo kwangu limekuwa bao bora nililofungwa,” alisema na kuongeza;
“Maneno yamekuwa mengi kwangu eti nimeruhusu mabao ya kizembe, naheshimu mitazamo na mawazo ya kila mmoja wao kwani kazi yangu naamini naifanya vyema.”
Kwa upande wa Kocha Msaidizi wa kikosi hicho, Awadhi Juma ‘Maniche’ alisema hawezi kutoa lawama kwa mtu yoyote katika mchezo huo kwa sababu walifungwa na timu bora kutokana na makosa binafsi hivyo wanarudi uwanja wa mazoezi ili kufanyika kazi yasijirudie.
Kipigo hicho kinaifanya Mtibwa Sugar kushika nafasi ya sita na pointi zake saba kwenye msimamo baada ya kucheza michezo minne.