Anatosha! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya mashabiki, wapenzi na baadhi ya mastaa wa zamani wa kikosi cha Simba kuridhishwa na ubora wa Kocha Juma Mgunda.
Mgunda aliyekuwa kocha wa Coastal Union, aliteuliwa na Simba Septemba 7, kocha mkuu wa muda wa timu hiyo akirithi mikoba ya Zoran Maki aliyeondoka kufuatia makubaliano ya pande zote mbili.
Kwa muda mfupi akiwa Simba, Mgunda ameiongoza timu hiyo katika michezo miwili akishinda yote ugenini, akianza kwa ushindi wa 2-0 dhidi ya Nyasa Big Bullets ya Malawi katika mtanange wa hatua ya awali Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya juzi kushinda 1-0 mbele ya timu ngumu ya Tanzania Prisons.
Mmoja ya waliomkubali Mgunda apewe mikoba kamili ni winga wa zamani wa Simba, Mnenge Suluja aliyesema mabosi wa timu hiyo wamwamini kocha huyo na kumkabidhi silaha zote ili aiwezeshe kufanya vizuri baada ya kusuasua kwa muda.
“Nashauri tu wakae na Mgunda na hata ikiwezekana mpaka mwisho wa msimu huu, anafaa kwa sababu kwanza ana elimu ya kutosha alikuwa na wachezaji wa Coastal na ikafanya vizuri,” alisema Suluja, kuongeza;
“Kama ukimpa Mgunda hao mapro (nyota wa kigeni) atafanya vizuri zaidi, kikubwa tu uongozi na mashabiki na wanachama wa Simba wampe ushirikiano hiyo kazi sio ya mtu mmoja ni ya kushirikiana kwa pamoja.”