Mpaka mechi ya juzi jioni baina ya Simba na Prisons inaanza hakukuwa na kocha mzawa aliyekuwa ameomba kuifundisha klabu hiyo.
Simba iko kwenye harakati za kutafuta kocha mkuu atakayerithi mikoba ya Zoran Maki aliyeachana nayo siku kadhaa zilizopita.
Simba imempa kazi ya muda mzawa Juma Mgunda kukaimu nafasi hiyo, ambaye aliiongoza kushinda mabao 2-0 kwenye mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu dhidi ya wenyeji, Nyasa Big Bullets nchini Malawi na jana ikashinda bao 1-0 dhidi ya Tanzania Prisons katika Ligi Kuu.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally, Mgunda bado hajapewa mkataba na klabu hiyo ambayo baada ya kupata kocha mkuu itaamua kama nyota wa zamani wa timu ya taifa atasalia kwenye timu kama kocha msaidizi sanjari na Suleiman Matola au itaamuliwa vinginevyo.
Ahmed alisema jana kwamba mchakato wa klabu kupata kocha mkuu unaendelea na baadhi ya makocha kutoka nchi za Ulaya wameomba nafasi hiyon ingawa hakuwaweka wazi kwa madai kwamba bado hawajapata chaguo halisi na lolote linaweza kutokea muda wowote kwavile kila muda maombi yanatiririka. “Makocha wengi wameomba, wengi wao ni kutoka nchi za bara la Ulaya, makocha wetu wazawa hadi sasa hakuna aliyekuomba nafasi hiyo, kama klabu imepanga zoezi la kupata kocha mkuu likamilike mapema kwa kuwa timu hiko kwenye mashindano.
“Tunatarajia mchakato huo ukamilike mapema na kuwa na kocha mkuu, ambaye ataendeleza pale Mgunda atakapokuwa amefikia kwa kuwa hivi sasa yeye ni kocha mkuu wa muda,”alisema ingawa viongozi wa juu jana walikuwa wagumu kuzungumzia mchakato huo kwa madai kwamba bado wanaendelea kuchekecha.
Kuhusu Mgunda kutokuwa na mkataba Simba, Ahmed alisema ni kweli bado hajapewa, lakini itaamuliwa na uongozi kama atapewa mkataba utakuwa ni wa muda gani.
“Ni kweli hajapewa mkataba bado, lakini kama nilivyosema atakapoajiriwa kocha mkuu, klabu itaangalia uwezekano wa kuwa na makocha wasaidizi wawili, Mgunda na Matola au vinginevyo,” alisema.