Beki wa zamani wa Yanga, Muarami Issa ‘Marcelo’ ameukubali mziki wa timu hiyo huku akiipa nafasi ya kushinda katika mchezo wa leo dhidi ya Zalan ya Sudan Kusini na kufanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa msimu huu.
Yanga itaikaribisha Zalan ya Sudan Kusini leo Jumamosi saa 1 usiku katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam kwa mchezo wa marudiano hatua ya awali ligi ya mabingwa barani Afrika baada ya Wana Jangwani kuibuka na ushindi wa mabao 4-0 katika mchezo wa kwanza.
Marcelo ambaye aliitumikia Yanga msimu wa mwaka 2019/2020 alijiunga nayo akitokea Malindi ya Zanzibar lakini dirisha dogo akapelekwa Singida United kwa mkopo ambao baada ya kumalizika hakurejea tena Jangwani.
Beki huyo wa kushoto kwa sasa anakipiga Pamba SC ya Mwanza inayoshiriki Championship (zamani daraja la kwanza) ambapo amekisifu kikosi cha Yanga kwa ubora ilionao kulinganisha na wakati akiichezea timu hiyo huku akiwapa nafasi kubwa ya kufanya vizuri.
Amesema ubora wa wachezaji, muunganiko na usajili uliofanyika kuongeza makali unawapa nafasi kubwa ya kuendelea kutamba nchini na kimataifa huku akieleza kuwa ushindi wa mchezo wa mkondo wa kwanza walioupata umewapa nguvu na hamasa ya kushinda kesho.
“Nafikiri kwamba hata walichokifanya mechi ya kwanza dhidi ya Zalan ni kizuri kimewapa hamasa wachezaji na mashabiki,”
“Kwa sasa wana nafasi kubwa ya kufanya vizuri sana kwa sababu timu iko katika rythm nzuri ina wachezaji bora na wazuri kwahiyo naamini itafanya vizuri na inaweza kufika mbali kimataifa,”