Home Habari za michezo DUH…KWA HILI, KISINDA NDIO BASI TENA YANGA….KIGOGO MKUBWA AFICHUA NAMNA WALIVYOCHEZA PATA...

DUH…KWA HILI, KISINDA NDIO BASI TENA YANGA….KIGOGO MKUBWA AFICHUA NAMNA WALIVYOCHEZA PATA POTEA NYINGI…


Sinema ya winga wa Yanga, Tuisila Kisinda bado inaendelea. Kocha Nabi Mohammed amefunguka kilichotokea na alichofanya lakini Mkurugenzi wa Mashindano wa klabu hiyo, Saad Kawemba ametoa mpya. Lakini kanuni nazo zimeongea.

Iko hivi; Yanga imeanza kasi ya kuelekea kwenye hatua kutinga makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika huko Februari mwakani na ikiwa hilo litatimia kwa kuwatoa Zalan kisha mshindi dhidi ya St. Georges/Al Hilal, watapiga ndege watatu kwa jiwe moja.

Kwanza watavunja mwiko wa miaka 23 wa kucheza mashindano hayo bila kutinga hatua hiyo kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika lakini pili watajihakikishia donge nono la Dola 550,000 (Sh 1.3 bilioni) ambalo kila timu inayotinga hatua hiyo inavuna kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf).

Jambo la tatu ambalo mashabiki wa Yanga bila shaka watapenda kulisikia ni kwamba katika hatua hiyo ndio wataanza rasmi kumtumia winga wao kipenzi, Tuisila Kisinda waliyemrejesha kutoka RS Berkane ya Morocco.

Baada ya sintofahamu ya siku kadhaa juu ya uhamisho wa winga huyo kutoka DR Congo, ni wazi sasa kuwa Yanga ina nafasi finyu ya kumtumia Kisinda kwenye mechi za Ligi Kuu na katika mashindano ya kimataifa.

Kwa mujibu wa viongozi nyota huyo ataanza kuonekana uwanjani kwenye Ligi Kuu ya NBC baada ya dirisha dogo la usajili kuanzia Desemba 15 mwaka huu na katika Ligi ya Mabingwa Afrika kuanzia hatua ya makundi inayoanza Februari 2023.

Licha ya uongozi wa Yanga kufanya jitihada kubwa kuhakikisha Kisinda anapewa usajili na kuitumikia timu hiyo ikiwemo hadi kulipa faini ya fedha Caf, mambo bado ni magumu.

Mkurugenzi wa mashindano wa Yanga ambaye amebobea kwenye soka la Afrika, Saad Kawemba amekiri kuwa hawataweza kumtumia Kisinda hadi katika hatua ya makundi ya mashindano ya klabu Afrika.

“Ni kweli tumelipia na jina lake halipo, sio rahisi kuingiza jina moja kwa moja, kwasababu tumelipia jina lake limewekwa pembeni litaingizwa kwenye majina ya timu hatua inayofuata,” alisema Kawemba.

SOMA NA HII  SENZO: YANGA ITAREJEA KWENYE UBORA

Kauli hiyo ya Kawemba imekuja wakati kocha Nasreddine Nabi akifichua kuwa; “Tulituma barua ya maombi TFF kwaajili ya kuwaomba kuondoa jina la Lazarous Kambole ambaye ana majeraha ya muda mrefu na kuingizwa jina la Kisinda ambaye tunaamini atatumika muda wote kutokana na kuwa kwenye hali nzuri.

“Ombi letu hadi sasa bado hatujapata majibu tunasubiri ili kufahamu kama ataweza kutumika,” alisema Nabi na kuongeza kuwa mchezaji huyo yuko vizuri na muda wowote akiruhusiwa atamuanzisha.

KANUNI ZIKOJE

Matakwa ya kikanuni za Ligi Kuu ya NBC, Ligi ya Mabingwa Afrika na muongozo wa hadhi za wachezaji na uhamisho wa wachezaji ndio yaliyokwamisha uwezekano wa Kisinda kuitumikia Yanga kwa sasa.

Yanga ilitaka kulisajili jina la Kisinda kwa ajili ya kuchukua nafasi ya Kambole ambaye ilipanga kumuacha kwa sababu ya majeraha ya muda mrefu.

Hata hivyo kwa mujibu wa muongozo wa hadhi na usajili wa wachezaji wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA), mkataba wa mchezaji hauwezi kusitishwa wakati msimu umeshaanza, hilo likifafanuliwa katika kanuni ya 16.

Wakati Yanga wanataka jina la Kambole liondolewe, tayari msimu wa Ligi Kuu ya NBC ulikuwa umeshaanza na kwa ajili ya hilo kutimia, ilipaswa awe amehamishwa kwa mkopo kwenda klabu nyingine jambo ambalo halikufanyika kwa wakati.

Ibara ya pili ya kanuni ya tano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, inafafanua kuwa mchezaji ili aruhusiwe kuitumikia klabu katika mashindano hayo, anapaswa kuwa na leseni ya kushiriki mashindano ya ndani kwa nchi ambayo klabu iliyomsajili ipo.