Home Habari za michezo KUELEKEA MECHI YA CAF….WAFAHAMU WAPINZANI WA SIMBA NYASA BIG BULLETS…HAWAJAWAHI KUFUNGWA KWAO..

KUELEKEA MECHI YA CAF….WAFAHAMU WAPINZANI WA SIMBA NYASA BIG BULLETS…HAWAJAWAHI KUFUNGWA KWAO..


Simba itakuwa na kibarua kigumu leo kwenye Uwanja wa Taifa wa Bingu, jijini Lilongwe, kutokana na rekodi ya wenyeji wao, Nyasa Big Bullets, ambao wanatetea ubingwa wao wa ligi yao ya ndani ‘TNM’, ambayo ipo raundi 20 bila ya kupoteza.

Simba ikiwa na kocha wake wa muda, Juma Mgunda iliondoka nchini jana, kwenda Malawi kupigania nafasi ya kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku kukiwa na matumaini ya kufanya vizuri.

Wakati Simba ikiwa na matumaini hayo, Mgunda atatakiwa kufanya kazi ya ziada maana wenyeji wao kwenye ligi ya ndani, wameshinda michezo 16 na kutoka sare nne, huku kwenye mchezo wao wa mwisho, Agosti 28 wakiitandika TN Stars mabao 8-0.

Miongoni mwa wachezaji wao hatari ni pamoja na Anthony Mfune, ambaye kwenye mchezo wa mwisho wa ligi alifunga mabao matatu ‘hat-trick’.

Takwimu zinaonyesha kuwa Nyasa Big Bullets imefunga mabao 46 kwenye ligi, ina wastani wa kufunga mabao mawili kwenye kila mchezo, imeruhusu 11, inaonekana kuwa wanaukuta na safu nzuri ya ushambuliaji.

Nyasa Big Bullets ilianzishwa 1967 na kundi la vijana wa mtaani la Mighty Wanderers ikifahamika kama Nyasaland Bullets, ilipata ufadhili kutoka kwa Kampuni ya Bata Shoe na ilibadilishwa jina na kuitwa Bata Bullets.

Msimu wa 1970 ulikuwa wa mafanikio makubwa kwani Bullets ilitwaa mataji matatu Ligi ya Soka ya Blantyre na Wilaya (BDFL), Kombe la Chibuku na Kombe la Castle.

2003, Rais wa wakati huo wa Malawi, Bakili Muluzi alipitisha timu hiyo na kuipa jina la Bakili Bullets. Ilikuwa katika kipindi ambacho timu ilifurahia mojawapo ya vipindi vyake vya kupendeza, kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Shauku ya kutaka kufanya vizuri katika mashindano hayo ya kimataifa klabu hiyo iliweka kambi ya mazoezi nchini Uingereza, lakini mambo yalikwenda tofauti. Kwa sasa timu hiyo inafadhiliwa na Kampuni ya Nyasa Manufacturing (NMC).

Bullets inanolewa na kocha wa zamani wa timu ya Taifa ya Zimbabwe, Callisto Pasuwa, huku msaidizi wake akiwa nahodha wa zamani na beki wa timu ya Taifa ya Malawi, Peter Mponda.

SOMA NA HII  'KICHWA DONGO' CHAMA NAYE AVUNJA UKIMYA KUHUSU MASTAA WAPYA SIMBA...AJITOLEA MFANO MWENYEWE...