Home Simba SC KWA HILI TIZI LA GOMES.. HAO AL AHLY WAJIANDAE “KUCHAKAA” KWA MKAPA

KWA HILI TIZI LA GOMES.. HAO AL AHLY WAJIANDAE “KUCHAKAA” KWA MKAPA


Juzi Ijumaa, Simba ilifanya mazoezi huku kocha wake, Didier Gomes akiwa na furaha baada jeshi lake kukamilika akiamini kama wote wataendelea kuwa fiti hadi Jumanne ana uhakika wa kuimaliza Al Ahly iliyotua nchini usiku wa kuamkia jana.

Katika mazoezi hayo Gomes aliwagawa wachezaji wake katika makundi mawili, 11 wa kwanza kwenda kufanya mazoezi ya nguvu (gym) waliosimamiwa na kocha wa viungo, Adel Zrane.

Kundi hilo walikuwepo, Clatous Chama, Luis Miquissone, Aishi Manula, Pascal Wawa, Said Ndemla, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Gadiel Michael, Mzamiru Yassin, Meddie Kagere, Joash Onyango na Shomary Kapombe.

Kundi jingione lilibaki mikononi mwa Gomes na msaidizi wake, Seleman Matola kwa kufanya tizi uwanjani wakiwafanyisha mazoezi ya nguvu, kukimbia kwa muda mrefu na kuruka viunzi.

Gomes aliwataka wachezaji wao wakimbie kwa mbio ndefu kuzunguka uwanja mzima pamoja na zile fupi aina mbalimbali ambazo walikuwa wakipangiwa, baada ya hapo walifanya mazoezi ya nguvu ikiwemo kutumia vifaa na mwisho walimalizia kwa mazoezi ya viungo huku wakigusa mpira kwa muda mfupi tu.

Baada ya mazoezi hayo alisema baada ya kuwafuatilia vya kutosha Al Ahly wanatakiwa kufanya mazoezi mengi ya kutosha tena yenye kutengeneza nguvu ya kila mchezaji kwa muda mrefu kwani watakuwa wakipambana muda wote.

“Mechi hiyo itakuwa ya kushindana muda mwingi kutokana na ubora wa wapinzani wetu na ili tupate matokeo mazuri tunatakiwa kupambana bila kuonyesha kuchoka ndio maana tumeanza na kufanya mazoezi ya nguvu,” alisema Gomes.

SOMA NA HII  TSHABALALA AFUNGUKA KILICHOWAPONZA SIMBA