Home Uncategorized FAINALI YA KIBABE LEO AFCON, SENEGAL V ALGERIA

FAINALI YA KIBABE LEO AFCON, SENEGAL V ALGERIA


MCHEZO wa fainali ya michuano ya Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) kati ya Senegal na Algeria, unachezwa leo Ijumaa kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Cairo uliopo Cairo, Misri.

Awali mchezo huo ulipangwa kuchezeshwa na mwamuzi wa kati Victor Gomes raia wa Afrika Kusini, lakini yamefanyika mabadiliko na sasa atakuwa Sidi Alioum raia wa Cameroon.
Senegal licha ya muda mrefu kuwa na kikosi kizuri, lakini haikuwahi kushinda ubingwa wa Afcon, huku Algeria yenyewe ikiwa imebeba taji hilo mara moja, mwaka 1990.
Mashabiki wa soka wanauchukuliwa mchezo huu kama ni vita ya Liverpool dhidi ya Manchester City kwa maana ya kwamba, Sadio Mane wa Senegal, anaiwakilisha Liverpool na Riyad Mahrez upande wa Algeria, anasimama kama mpambanaji wa Manchester City.
 Nyota hao wawili, msimu uliopita wa 2018/19 katika Ligi Kuu England, timu zao za Liverpool na Man City, zilikuwa zikiwania ubingwa wa ligi hiyo na siku ya mwisho, Mahrez akiwa na kikosi cha Man City, wakawa mabingwa.
Kikubwa zaidi ni kwamba, timu hizi zote ni ngumu kufungika tangu kuanza kwa michuano hii. Senegal mpaka sasa imecheza mechi sita, imeruhusu kufungwa bao moja pekee, huku yenyewe ikifunga mabao nane.
Algeria katika mechi sita ilizocheza, imefunga mabao 12 na kuruhusu kufungwa mabao mawili.
SAFARI ZAO
Senegal mpaka kufikia fainali, imecheza jumla ya mechi sita, imeshinda tano na kufungwa moja dhidi ya Algeria. Matokeo ya mechi hizo ni; Senegal 2-0 Tanzania, Senegal 0-1 Algeria, Kenya 0-3 Senegal, Uganda 0-1 Senegal, Senegal 1-0 Benin na Senegal 1-0 Tunisia.
Algeria yenyewe katika mechi hizo sita, imeshinda zote ikiwemo moja dhidi ya Senegal kwenye hatua ya makundi iliposhinda 1-0.
Matokeo yake ya jumla ni; Algeria 2-0 Kenya, Senegal 0-1 Algeria, Tanzania 0-3 Algeria, Algeria 3-0 Guinea, Ivory Coast 1-1 Algeria (Algeria ikashinda kwa penalti 4-3) na Algeria 2-1 Nigeria.
KUKUTANA KWAO
Katika mechi nne zilizopita baina ya timu hizo mbili kwenye Afcon pekee, Algeria haijapoteza hata moja. Imeshinda tatu na sare moja.
Matokeo ya mechi hizo ni Algeria 2-1 Senegal, Senegal 0-2 Algeria, Senegal 2-2 Algeria na Senegal 0-1 Algeria.
WATAKAOKOSEKANA
Senegal itamkosa beki wake, Kalidou Koulibaly ambaye ana kadi mbili za njano. Wakati Algeria muziki wao utakuwa kamili.
KAULI ZA MAKOCHA
Kitu ambacho wengi wanapaswa kukifahamu ni kwamba, fainali hii inawakutanisha makocha wazawa. Senegal inanolewa na Aliou Cisse raia wa nchi hiyo, kama ilivyo kwa Algeria ambapo kocha wao ni Djamel Belmadi.
Cisse anasema: “Najisikia furaha sana, hatukuwahi kucheza fainali kwa kipindi cha miaka 17, hiki kilichotokea sasa ni matunda ya maandalizi ya muda mrefu.
“Mchezo wa fainali ni michezo kama mingine ingawa ina utofauti wake, naamini ushindani utakuwa mkubwa kwa sababu sisi sote lengo letu ni moja, kuwa mabingwa.”
Naye Belmadi anasema: “Matokeo mazuri ya fainali ni kushinda na si kucheza tu. Tupo hapa kwa sasa na sisi sote tunahitaji kombe. Tunakutana na wapinzani ambao nao wanahitaji kombe, hivyo utakuwa mchezo mgumu sana.
“Kwa sasa ujumbe uwafikie viongozi wa soka katika bara hili, makocha vijana tena wazawa wanaweza kuandika historia na kuwatengeneza wachezaji wazuri.
“Aliou Cisse ni rafiki yangu mkubwa sana, nakwenda kupambana naye. Tofauti yetu kubwa ni kwamba, yeye anainoa Senegal kwa kipindi cha miaka minne sasa, mimi ndiyo kwanza nina mwaka mmoja hapa. Naweza kusema ni kocha mzuri na anaifanya kazi yake vizuri sana.”
“Nawaahidi Waalgeria nitawapa kila wanachokihitaji ili kuwafanya wawe na furaha, lakini siwezi kuwaahidi ubingwa kwa sababu haupo mikononi mwangu.”
SOMA NA HII  OKWI KURUDI MSIMBAZI..? HANS POPE AMEFUNGUKA HAYA..!!