Home Habari za michezo MIEZI MIWILI KABLA YA KOMBE LA DUNIA….HAWA HAPA MASTAA 10 AMBAO ITAKUWA...

MIEZI MIWILI KABLA YA KOMBE LA DUNIA….HAWA HAPA MASTAA 10 AMBAO ITAKUWA MARA YAO YA MWISHO KUCHEZA SOKA…


Kombe la Dunia la FIFA la 2022 liko karibu kabisa. Tumebakiza miezi miwili kabla ya mchezo wa ufunguzi wa mashindano hayo makubwa zaidi yanayofanyika kila baada ya miaka minne kuanza.

Kombe la Dunia bila shaka ni tukio kubwa zaidi la soka duniani na ni ndoto ya kila mchezaji kuwakilisha taifa lake.

Ni timu bora pekee duniani ambazo zimefuzu kwa Kombe la Dunia. Tutazikosa timu bora kama Italia, Colombia, Sweden, Chile na Nigeria, ukizitaja kwa uchache ambazo zimeshindwa kufuzu.

Baadhi ya nyota wakubwa wa soka kama Erling Haaland, Mohamed Salah, Marco Verratti na David Alaba, ni miongoni ambao hawatashiriki Kombe la Dunia la 2022 baada ya timu zao za taifa kushindwa kufuzu.

Kombe la Dunia la 2022, ambalo litafanyika nchini Qatar, pia huenda likawa mara ya mwisho kuwaona baadhi ya wachezaji wakubwa wanaotawala soka la kisasa duniani.

Hapa tunawaangalia wanasoka nyota 10 ambao michuano hii inaweza kuwa ya mwisho kwao kuzichezea nchi zao, haya sasa…

#10. Edinson Cavani (Uruguay)

Edinson Cavani ni mmoja wa washambuliaji bora wa kizazi chake. Mchezaji huyu wa kimataifa wa Uruguay, amefunga mabao 56 na kutoa pasi za mabao 17 katika mechi 129 alizocheza hadi sasa katika timu yake ya taifa. Cavani anafahamika kwa uwezo wake wa kumalizia na kuongoza vizuri, pia anasifika kwa ukakamavu wake na ari yake ya kuipigania nchi yake.

Ana umri wa miaka 35 sasa na Kombe la Dunia la FIFA la 2022 huenda likawa la mwisho kwake. Cavani, ambaye aliondoka Manchester United baada ya mkataba wake kumalizika mapema msimu huu wa majira ya joto, kwa sasa ni mchezaji huru.

#9. Luis Suarez (Uruguay)

Mshambuliaji patina wa Cavani, Luis Suarez pia ni mchezaji bora wa kisasa. Suarez pia ana umri wa miaka 35 na kwa sasa anaitumikia klabu ya Nacional ya nchini Uruguay. Yeye ni mmoja wa washambuliaji wazuri zaidi wa zama za kisasa na amewatia hofu mabeki wengi wa Ulaya akiwa katika ubora wake.

Suarez amepita miaka yake ya kilele sasa na kiwango chake kimeshuka katika misimu ya hivi karibuni. Kwa hiyo, Kombe la Dunia la FIFA la 2022 huenda likawa la mwisho kwa El Pistolero huyo.

#8. Angel Di Maria (Argentina)

Angel Di Maria amekuwa mmoja wa wachezaji muhimu zaidi wa Argentina katika muongo mmoja uliopita. Kutokuwapo kwake kutokana na jeraha kunatajwa na wengi kama sababu kuu iliyoifanya Argentina kushindwa kuifunga Ujerumani katika fainali ya Kombe la Dunia la FIFA la 2014.

Di Maria alifunga bao la ushindi la La Albiceleste hao katika fainali ya 2021 ya Copa America. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 34, alijiunga na Juventus kama mchezaji huru mapema msimu huu wa majira ya joto na ingawa hayuko kwenye kilele cha uwezo wake, bado ni mwanasoka mzuri sana.

Lakini hakuna uwezekano wa kuwapo kwenye michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2026.

#7. Marco Reus (Ujerumani)

Marco Reus bila shaka ni mmoja wa washambuliaji bora wa kizazi chake. Kwa bahati mbaya, ushiriki wake katika timu ya Taifa ya Ujerumani umekuwa mdogo kutokana na majeraha. Ameichezea mara 48 pekee katika maisha yake ya soka, akifunga mabao 15 na kutoa pasi 14 za mabao.

Reus amecheza mechi tatu pekee kwenye Kombe la Dunia na atakuwa na matumaini ya kushiriki kwa kiasi kikubwa wakati huu. Hii inaweza kuwa nafasi ya mwisho ya mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 33, kucheza katika mashindano hayo.

SOMA NA HII  FT:GEITA GOLD 0 - 5 SIMBA SC.....KIBU DENIS AMPIGA BUSU CHAMA...SAKHO KAMA MESSI VILEE...

#6. Thiago Silva (Brazil)

Brazil haina upungufu wa walinzi wa kiwango cha kimataifa kuelekea Kombe la Dunia la FIFA 2022. Beki huyo wa kati wa Chelsea mwenye umri wa miaka 37, atakuwa mtu wao mkuu katika safu ya tatu ya ulinzi. Mkongwe wa mchezo huo, Silva bado ni ‘mnyama’ kabisa nyuma ingawa anakaribia miaka 40. Huenda hili likawa Kombe la Dunia la mwisho la Silva na Brazil.

#5. Thomas Muller (Ujerumani)

Thomas Muller ni nyota kwa kikosi cha Ujerumani. ‘Mfalme wa asisti’ wa Ulaya ni mmoja wa wanasoka wenye kipaaji cha kiufundi na akili kwenye sayari hii. Fowadi huyo wa Bayern Munich anaendelea kufanya kazi kwa kiwango cha juu licha ya kuwa amebakisha wiki chache tu afikishe umri wa miaka 33.

Katika mechi 16 za Kombe la Dunia kwa Ujerumani, Muller amefunga mabao 10 na kutoa asisti sita. Namba hizi ni ushahidi wa jinsi mshambuliaji huyo mkongwe alivyo muhimu kwa timu ya Taifa ya Ujerumani.

#4. Karim Benzema (Ufaransa)

Karim Benzema alirudishwa katika timu ya Taifa ya Ufaransa mwaka 2021 baada ya kukosekana kwa miaka sita. Mfaransa huyo amekuwa katika kiwango cha hali ya juu katika klabu ya Real Madrid hivi karibuni na mambo makubwa yanatarajiwa kutoka kwake kwenye Kombe la Dunia la FIFA la 2022.

Hata hivyo, Benzema ana umri wa miaka 34 sasa na huenda hii ikawa mara yake ya mwisho kucheza Kombe la Dunia. Ni mmoja wa washambuliaji walio katika kiwango bora zaidi duniani na anaweza kuwa nyota muhimu zaidi kwa mafanikio ya Ufaransa.

#3. Luka Modric (Croatia)

Luka Modric alishinda Mpira wa Dhahabu, tuzo kwa mchezaji bora wa mashindano, katika Kombe la Dunia la FIFA la 2018. Aliiongoza Croatia kutinga fainali miaka minne iliyopita, ambapo hatimaye walipoteza kwa Ufaransa. Modric atakuwa na umri wa miaka 37 wakati Kombe la Dunia la FIFA 2022 linaanza.

Hata hivyo, amekuwa katika kiwango cha hali ya juu kule Real Madrid hivi karibuni na kwa mara nyingine atakuwa mchezaji mkuu wa Croatia.

#2. Lionel Messi (Argentina)

Lionel Messi ndiye mwanasoka bora zaidi wa wakati wote. Mshindi huyo wa tuzo ya Ballon d’Or mara saba amekuwa katika daraja la aina yake katika maisha yake yote. Alitawazwa ‘Mchezaji Bora wa Mashindano’ kwenye Copa America ya 2021 baada ya kuiongoza Argentina kutwaa taji hilo kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1993.

Messi amefunga mabao 86 na kutoa asisti 51 katika mechi 162 alizoichezea ‘La Albiceleste’ katika maisha yake ya kimataifa. Kombe la Dunia ndilo taji pekee ambalo halipo kwenye kabati lake la mataji. Michuano hii itakuwa ya mwisho kwake, kwa sababu hivi sasa ana umri wa miaka 35.

#1. Cristiano Ronaldo (Ureno)

Cristiano Ronaldo ndiye mfungaji bora wa muda wote katika soka la kimataifa la wanaume. Amefunga mabao 117 na kutoa asisti 42 katika mechi 189 alizoichezea timu ya Taifa ya Ureno. Ronaldo ni mmoja wa wanasoka bora wa wakati wote.

Watu watammisi sana atakapoamua kutundika daluga zake. Ronaldo sasa ana umri wa miaka 37 na hakuna uwezekano wa kuwapo kwenye Kombe la Dunia la FIFA 2026.