Home Habari za michezo PAMOJA NA MGUNDA KUANZA VIZURI SIMBA…BARBARA AISHINDWA KUJIZUIA…AANIKA YA MOYONI KUHUSU NAFASI...

PAMOJA NA MGUNDA KUANZA VIZURI SIMBA…BARBARA AISHINDWA KUJIZUIA…AANIKA YA MOYONI KUHUSU NAFASI YAKE…

KAIMU Kocha Mkuu wa Simba, Juma Mgunda, ameonyesha kufurahia ushindi wa mabao 2-0 kwenye mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Nyasa Big Bullets ya Malawi timu yake ikiwa ugenini baada ya kueleza kuwa kazi haijaisha, huku Ofisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Barbara Gonzalez akiwasifu makocha wazawa kwa kuiongoza vema timu hiyo.

Mbali na hayo, straika Moses Phiri aliyefunga bao la kwanza kwenye mechi hiyo, aliwasifu wanachama na mashabiki wa Simba kwa kusafiri kwa umbali mrefu kuwapa sapoti, akiahidi hatowaangusha kwenye mechi ya marudiano.

Wote hao walizungumza juzi baada ya Simba kumaliza dakika 90 kwenye Uwanja wa Bingu Mutharika kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya wenyeji hao, yakiwekwa wavuni na Phiri, pamoja na nahodha wa kikosi hicho, John Bocco.

“Nina furaha kwa sababu nimeshinda ugenini, lakini mechi haijaisha mpaka iishe kule nyumbani, tumeyaona makosa ya wachezaji, tunakwenda kuyarekebisha ili tushinde. Kwenye mechi chochote kinaweza kutokea, iwe nyumbani au ugenini, siwezi kuidharau Nyasa Big Bullets. Muhimu kwa sasa ni kwamba tunaongoza, lakini tuna mechi nyingine nyumbani na tuna mtaji wa mabao 2-0,” alisema Mgunda ambaye ilikuwa ni mechi yake ya kwanza kuiongoza Simba kwenye maisha yake ya soka.

Alimsifu kocha aliyemkuta Selemani Matola, akidai kuwa amempa mwanga wa kuwafahamu wachezaji na kuwatumia.

“Nimeipokea timu muda mfupi sana kabla ya mechi, lakini mwalimu niliyemkuta nimeshawahi kufanya naye kazi timu ya Taifa, Taifa Stars miaka miwili au mitatu, najua uwezo wake, nilianzia pale aliponiambia timu ikoje. Amenisaidia kunipa mwanga kuhakikisha timu inafanya vizuri,” alisema kocha huyo wa zamani na mchezaji wa Coastal Union.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Barbara aliwasifu wachezaji na benchi lote la ufundi kwa kuiheshimisha Simba na nchi kwa ujumla.

“Tunashukuru walimu na wachezaji kuiheshimisha klabu kupambana, kucheza kwa nembo ya Simba na Tanzania, bado tuna safari ndefu kuna dakika 90 za nyumbani na tunategemea kuona ushindi zaidi ili twende kwenye raundi nyingine, nimefurahi kuona makocha Watanzania wameleta ushindi kwenye mechi ya ugenini.”Pia nitoe pongezi kwa wanachama na mashabiki na kuwashukuru pia kwani wamesafiri saa 40, na zaidi ya watu 150 kutoka Tanzania wamekuja hapa kuipa sapoti timu, wameonyesha mapenzi ya dhati na imetusaidia, ndiyo maana unaona hata wachezaji wetu wamepambana sana kwa sababu walikuwa wanasikia makelele na ngoma za nyumbani kutoka kwa mashabiki tokea hotelini hadi uwanjani,” alisema.

SOMA NA HII  HAPA SIMBA WAVUNJE TU BENKI MAANA SIO KWA DAU HILI

Phiri, mfungaji wa bao la kwanza alisema huo ni mwanzo tu, huku akikiri kuwa mashabiki wengi waliojitokea kuwashangilia walikuwa chachu ya ushindi huo.

“Nafikiri huu ni mwanzo mzuri kwetu hasa kushinda mechi ya ugenini, tumekuja kushinda na lengo letu limetimia.

“Nashukuru kwa kufunga na kwa hii imekuja kwa ushirikiano wa wachezaji wenzangu, najua kuna mashabiki wengi walikuja kutoka Tanzania kutupa sapoti, hiyo ilikuwa sababu ya kutusukuma na kujituma zaidi kwenye mechi hii na zingine zitakazokuja, nao wanatakiwa kuendelea kuja kutushangilia, hatutowaangusha,” alisema Mzambia huyo.

Kwa upande wa nahodha Msaidizi wa Simba, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, alisema hawajamaliza kazi, wanarudi imara kwa ajili ya kutafuta matokeo chanya katika michezo iliyopo mbele yao ukiwamo huo wa marudiano.

Alisema baada ya kumalizana na Big Bullets sasa akili na nguvu zao wanazielekeza kwenda kutafuta pointi tatu katika mchezo ujao dhidi ya Tanzania Prisons ili kuendelea kubaki kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu.

“Ushindi muhimu ugenini tumejiandaa vema kwa mechi zetu zijazo ili kufikia malengo, asanteni mashabiki wetu kwa dua zenu na wale mliotoka Tanzania hadi Malawi sapoti yenu ilikuwa kubwa sana”.

Kikosi cha Simba baada ya kurejea kitashuka Uwanja wa Sokoine Jumatano kuvaana na Tanzania Prisons kabla ya kurejea Dar es Salaam kuisubiri Nyasa Big Bullets katika Uwanja wa Benjamin Mkapa Jumapili.