Wakati Simba ikitamba kuongoza ligi kwa mechi mbili za mwanzo, watani wao Yanga kumbe wala hawana presha kutokana na kujivunia rekodi bora ya msimu uliopita wakiamini watawanasa kiualini Wekundu hao wakati Ligi Kuu Bara ikirejea kuanzia wikiendi hii.
Yanga ilichukua ubingwa wa ligi msimu uliopita ikiweka rekodi nyumbani na ugenini huku pia ikipewa nafasi kubwa kuirudia msimu huu, ambapo ilianza kwa ushindi mechi mbili ugenini dhidi ya Polisi Tanzania na Coastal Union, waliowafunga 2-1 na 2-0 mtawalia.
Simba yenyewe ilishinda nyumbani kwa kuifumua Geita Gold mabao 3-0 na Kagera Sugar mabao 2-0, lakini wakati ligi ikirejea Wekundu watakuwa na kibarua kwa mechi za ugenini ilhali watani wao watakuwa wakirejea nyumbani na benchi la ufundi la timu hiyo limetamba kwamba wamejipanga kuweza kuweka heshima mechi hizo.
Mara Simba ikimalizana na KMC jijini Dar es Salaam Septemba 7, itasafiri hadi Mbeya kucheza mechi dhidi ya Tanzania Prisons na Mbeya City ambazo zote ilizipoteza msimu uliopita kwa bao 1-0 .
Baada ya mechi hizo mbili, Simba itarejea Dar es Salaam kuikabili Dodoma Jiji kisha itasafiri tena hadi Singida kucheza na Singida Big Stars, ilihali Yanga katika mechi nne kati ya tano itakazocheza kwenye ligi itakuwa Uwanja wa Benjamin Mkapa ambao umekuwa na rekodi tamu kwao.
Yanga itaanza mechi za nyumbani dhidi ya Azam (Septemba 6) kisha itaialika Mtibwa Sugar kabla ya kuvaana na Ihefu inayoutumia Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam kama wa nyumbani baada ya uwanja wao wa Highland Estate kufungiwa.
Baada ya mechi na Ihefu , Yanga itaikabili Namungo kwa mechi ya ugenini, japo itachezwa Uwanja wa Mkapa kama uwanja wa nyumbani wa Wauaji hao wa Kusini kutokana na uwanja wao wa Majaliwa, Ruangwa Lindi kuwa kwenye ukarabati.
Kocha Msaidizi wa Yanga, Cedrick Kaze alisema wanaendelea na maandalizi kujiweka fiti kwa mechi yao ya ligi dhidi ya Azam FC na ya kimataifa, lakini pia kwa michezo mingine iliyopo mbele yao.
“Timu inaendelea vizuri na mazoezi kila mchezaji anatambua michezo muhimu iliyo mbele yetu na tumecheza mchezo na KMC kirafiki ili kujiweka tayari dhidi ya Azam FC na mchezo wetu wa ligi ya mabingwa Afrika,” alisema Kaze
“Wachezaji wetu wapo kwenye hali nzuri hata waliokuwa majeruhi wamerudi mazoezini akiwemo Crispin Ngushi, Joyce Lomalisa na Lazarous Kambole wameanza mazoezi ya gym kurudisha utimamu wa mwili.”
Kaze alisema malengo yao msimu huu ni kuhakikisha wanatetea mataji yote wanayoyashikilia wakitambua ugumu wa mashindano ya ligi na kimataifa wanapopambana kuhakikisha wanaiweka sawa timu ili iendelee kuonyesha ushindani.
REKODI ZA YANGA
Mabao 49 iliyofunga msimu uliopita, 29 yalifungwa Kwa Mkapa wakati 20 ilifunga ugenini na katika mabao nane iliyofungwa matatu Kwa Mkapa na matano ugenini na kwenye pointi 74 ilizowapa taji kati ya hizo 40 ilizikusanya Uwanja wa Mkapa wakati 34 ikikusanya mkoani ambako ilishinda mechi 12 na kutoka sare nne.
REKODI ZA SIMBA
Kwa upande wa Simba wao kwenye michezo 15 waliyocheza mkoani imeshinda mechi nne tu, imetoka sare nane na kufungwa tatu ikikusanya pointi 20, mkoani imefunga mabao 14 huku ikifungwa mabao kumi.