Home news HIVI NDIVYO YANGA YA GSM WALIVYOPINDUA MEZA KIBABE USAJILI WA PHIRI…SIMBA WABAKI...

HIVI NDIVYO YANGA YA GSM WALIVYOPINDUA MEZA KIBABE USAJILI WA PHIRI…SIMBA WABAKI WAKILIA…


MASHABIKI wa Simba, bado hawaamini kama ni kweli mabosi wa timu hiyo wamepigwa bao na wenzao wa Yanga kwenye usajili wa mshambuliaji Mzambia, Moses Phiri.

Lakini ukweli ndio huo, Phiri amesainishwa mkataba wa awali wa miaka miwili ili atue Jangwani, baada ya mabosi wa klabu hiyo wakiongozwa na Injinia Said Hersi kufanya umafia wa aina yake, kupindua meza kibabe jioni kwa kuipora Simba nyota huyo, huku wakiipiga bao pia timu nyingine ya Afrika Kusini.

Kama Yanga itamshusha Phiri, mkasa wake utafanana kidogo na ule wa Rally Bwalya, Luis Miquissone na Henoc Inonga Baka walipotua Simba, kwani Yanga ilizungumza nao kila kitu, lakini ghafla wakaibukia Msimbazi na kuliamsha kinoma, huku wakiwaacha mashabiki wa Yanga wakishangaa tu.

Yanga imepindua meza na kuvamia dili la Mzambia huyo, hii hapa ni picha zima ilivyokuwa katika dili hilo la Phiri kubadili mawazo ya kutua Msimbazi au kwenda zake Afrika Kusini kama alivyokuwa amepanga.

SAA 19 ZA KIBABE

Inaelezwa Yanga imekamilisha dili la Phiri, ikimtumia mjumbe wa kamati ya usajili ya klabu hiyo, Injinia Hersi Said, ambaye alichomoka ghafla nchini kimya kimya na kwenda Zambia kuzungumza na nyota huyo pamoja na klabu ya Zanaco anayoichezea.

Kabla ya kuondoka nchini, Mwanaspoti linafahamu tayari Hersi alishapokea baraka zote kutoka kwa Kamati ya Ufundi ya Yanga, chini ya Mwenyekiti Dominic Albinius na kocha mkuu Nesreddine Nabi aliyeridhishwa na kiwango cha Mzambia huyo baada ya kuona mikanda yake ya video.

Hakuna aliyefahamu wapi Hersi yupo kuanzia Jumatatu ya wiki hii, ila inaelezwa baada ya kutua Zambia na kukutana na mabosi wa Zanaco, kisha kuongea na Phiri, taarifa zilivuja kuna kigogo wa Yanga yupo jijini Lusaka, Zambia akipambana kusaka saini ya mshambuliaji huyo.

Muda aliosafiri Hersi na kuzungumza na mabosi wa Zanaco na kukamilisha dili inaelezwa alitumia saa 19 kuanzia hiyo Jumatatu.

Hersi alitua jijini Lusaka mchana Jumatatu na kumalizana na mchezaji huyo na wakala wake ndani ya muda huo, kabla ya juzi kukwea pipa na kurejea kimyakimya akitua saa 1:30 usiku.

ZANACO YAGOMA, WASAUZI WATIBUA

Hata hivyo, Hersi hakupata kirahisi saini ya Phiri, kwani mambo mawili yaliweka ugumu ikiwemo kwanza klabu yake iliyosisitiza haiwezi kumuachia kirahisi na awali kutaka dau la usajili liongezeke.

SOMA NA HII  KUELEKEA MECHI NA SIMBA KESHO....'SURE BOY' AOMBA MSAADA WA MASHABIKI ...HASIRA ZA KIPIGO CHA VIPERS ZAMTIA 'WAZIMU'...

Zanaco imegoma kumuachia kwa sasa kwa vile timu yao ni kati ya zilizotinga makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika ikipangwa Kundi A.

Inaelezwa kuwa, Hersi alikuwa tayari anafahamu kwamba ipo klabu ya Sauzi inayoshiriki Ligi Kuu (PSL), ilikuwa inakaribia kutuma ofa kubwa ambayo ingezuia usajili huo wa Phiri kuja Tanzania.

Ndipo kigogo huyo ambaye pia ni mmoja wa Wakurugenzi wa GSM inayoidhamini Yanga, alitumia uzoefu wake kuwalainisha mabosi wa Zanaco, akitumia hatua ya ukaribu wao wa kuialika timu hiyo hivi karibuni kwenye Kilele cha Wiki ya Mwananchi kuipata saini hiyo.

Licha ya hivyo, Zanaco inaelezwa imeshikilia msimamo wa kuitaka Yanga isimchukue Phiri, licha ya kumalizana kwa vile mkataba wake umebakiwa na miezi sita kabla ya kumalizika.

SIMBA YASHTUKA JIONI

Wakati Hersi akiwa katika saa la mwisho kumaliza dili hilo la usajili, mabosi wa Simba nao walionekana kuhaha kulizuia, bila mafanikio, kwani tayari wakala wa Phiri alishamaliza biashara na Yanga, kisha akaamua kuzima simu kwa muda ili kukwepa usumbufu.

Simba imekuwa ikimsaka Phiri kwa kilichoelezwa dili lao la kumrejesha Clatous Chama kuonekana kuwa zito kutokana na Wamorocco wa RS Berkane kutaka mkwanja hata kama atakuja Msimbazi kwa mkopo na ilitakiwa ivunje mkataba wa nyota huyo mwenye miaka 28.

Juzi wakati Hersi akirejea nchini,  kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere III na alipoulizwa ishu hiyo, aliishia kucheka kila baada ya swali kisha kujibu kwa kifupi; “Mimi nilisafiri kwa shughuli zangu ndugu yangu na sasa nimerejea, hayo mambo mengine siyafahamu kwa sasa,” alisema Hersi akijaribu kuficha ukweli wa usajili huo.

Licha ya Hersi kufanya siri, lakini taarifa kutoka kutoka Zambia zinasema, kwamba Phiri amesaini mkataba wa awali wa miaka miwili ili kuja kuongeza nguvu kubwa katika safu ya ushambuliaji ya Yanga inayoongozwa na Fiston Mayele na kuziba nafasi ya Yacouba Songne aliye majeruhi.

 Phiri mwenye umri wa miaka 28, anacheza nafasi zote za mbele wingi ya kulia, kushoto na ushambuliaji.