Home Habari za michezo GAMONDI PRESHA TUPU, BAADA YA WABONGO KUMGEUZIA KIBAO YANGA

GAMONDI PRESHA TUPU, BAADA YA WABONGO KUMGEUZIA KIBAO YANGA

Habari za Yanga SC

Nilitegemea siku moja kocha wa mpira, Miguel Gamondi atafahamu vizuri tabia ya mashabiki na watu wa mpira hapa Bongo baada ya mwanzo wake mtamu ndani ya Yanga.

Kile alichokutana nacho mwanzoni kilikuwa hakitoshi kumfanya afanye mjumuisho wa hulka ya mashabiki wa Yanga na hata wa mpira wa miguu kwamba ni waungwana sana na wanauelewa mpira hivyo ataishi bila presha yoyote.

Kiufupi Wabongo sisi kwenye soka bila unafiki hatuendi na sio marafiki wa kudumu na hilo ukitaka kulipima ni pale ambapo timu haifanyi vizuri au haijafanya kile ambacho watu wanakitegemea.

Siku za mwanzo za Gamondi zilikuwa tamu sana, ukitaka ugombane na mtu yeyote wa Yanga basi fanya ukosoaji tu wa mambo yanayohusu timu na ufundi ungeona balaa lake. Gamondi alifanywa kama malaika hakosei na waliojaribu kuonyesha kasoro wakaambiwa wanatumika na upande wa pili.

Kumbe ile ilikuwa ni kwa sababu Yanga ilikuwa inapitia kipindi cha raha ambayo ilikuwa haijaisha baada ya kutoka kucheza Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na ilikuwa suala la muda tu kudhihirisha hilo.

Baada ya Yanga kutopata ushindi katika mechi tatu za makundi Ligi ya Mabingwa Afrika, leo Yanga wenyewe wanatuonyesha kasoro za Gamondi kwamba hatoi nafasi kwa wachezaji wengi wa Yanga na kuwatumia wachache kwenye kila mechi, wanatuambia hana mpango mbadala timu ikizidiwa na wengine wanatuambia kuwa kuna wachezaji anawapenda hata wakikosea au wasipocheza vizuri anawapanga.

Baadhi sasa wanaunga mkono kwamba Yanga inahitaji kusajili mshambuliaji wa kati wakati ndio haohao wiki chache zilizopita waliunga mkono kauli ya kocha huyo kuwa mabao sio lazima yafungwe na mshambuliaji.

Kiufupi kabla hata msimu haujafikia nusu, Gamondi ameshapunguza mawakili wake tofauti na ilivyokuwa mwanzoni, hao ndio Wabongo bwana.

Ni walewale ambao walisahau kuwa uongozi wa timu ulitangaza kuwa malengo yao ni kufika hatua ya makundi tu ya Ligi ya Mabingwa Afrika, leo wanamgeuka kocha kisa wameona hakuna urahisi wa kuingia robo fainali, hatua ambayo haikuwa lengo lao.

SOMA NA HII  KUELEKEA DABI YA KARIAKOO SIMBA WALAMBA DILI HILI LA KIBABE