Home Makala SIO ZENGWE…UCHAFU WA ZAHERA SI USAFI WA YANGA…

SIO ZENGWE…UCHAFU WA ZAHERA SI USAFI WA YANGA…

WIKI iliyopita nilimsikia Ofisa Habari wa Yanga, Ally Shaban Kamwe akirudiarudia kauli kuwa; ‘Namheshimu Zahera’, wakati akijibu hoja alizoibua kocha huyo Mcongo katika mahojiano na Kituo cha Redio cha EFM.

Ni kauli inayotumiwa sana na watu kutaka kuonyesha kuwa hoja fulani aliyoisema si sahihi, hivyo hataki kumwambia si sahihi kwa kuwa anamheshimu, ila maelezo yanayofuata huwa ni kuonyesha kilichosemwa si sahihi.

Lakini maelezo ya Kamwe hayakufuatiwa na maelezo sahihi dhidi ya yale aliyozungumzia Zahera kuhusu tabia za viongozi wa Yanga, hasa Rais na mwenendo wa wachezaji ambao alituhumu kuwa baadhi wamewakalia mabegani makocha hivyo wanafanya watakavyo.

Badala yake, Kamwe aliweka mlolongo wa maswali kuhusu Zahera, akimtaka aeleze majukumu yake kama Mkuu wa Programu za Vijana aliyatekeleza vipi nia yake ya kusimamia timu ya wanawake ameyaacha vipi.

Ni kweli inawezekana hakufanya vizuri katika maeneo hayo na pengine kuna tatizo kubwa lililoifanya klabu isimuongezee mkataba. Lakini hayo hayafanyi hoja alizozitoa zisiwe na nguvu na kwa kuwa hazijajibiwa, zinaendelea kuwa na nguvu hadi hapo zitakapotolewa ufafanuzi na mamlaka.

Kuna vitu vinaonekana bayana kama vile vya Rais wa Yanga, Injini Hersi Said kutaka kuonekana yuko karibu sana na timu pamoja na wachezaji. Mara kadhaa picha zimetumwa akiwa pamoja na wachezaji, wakati mwingine akishiriki mazoezi au kupiga danadana, huku picha nyingine zikimuonyesha amepozi na wachezaji nyota.

Ziko video zinazoonyesha akizungumza na wachezaji ndani ya vyumba vya kubadilishia nguo. Hii ni kuweka weledi kando na kudhani kauli ya Rais ndio inayoweza kuamsha ari ya wachezaji.

Kama hizo video huchukuliwa wakati wa mapumziko, basi ni hatari kwa maendeleo ya timu na kwa kiasi fulani vitendo hivyo hupunguza ufanisi wa kocha na hatimaye timu kwa ujumla. Kila kitu kina mipaka yake.

SOMA NA HII  SIMBA, YANGA JIKITENI KWENYE ISHU YA KIBIASHARA, POROJO MUDA WAKE UMEISHA