Kocha Mkuu wa Simba Sc, Juma Mgunda, amesema amembadilishia majukumu ya uchezaji kiungo wa timu hiyo, Augustine Okrah raia wa Ghana kutoka namba kumi nakumpeleka winga moja kwa moja ambapo anafanya vizuri.
Mghana huyo ni kati ya wachezaji wapya waliosajiliwa na Simba msimu huu kwa ajili ya kukiongezea nguvu kikosi hicho.
Kiungo huyo katika michezo mitatu iliyopita ya Ligi Kuu Bara, ameonekana kucheza kwa kiwango kikubwa, huku akifanikiwa kufunga bao moja.
Mgunda amesema wakati anapewa majukumu ya kukinoa kikosi hicho, alimkuta Okrah anacheza namba 10, lakini baada ya kumuona mazoezini haraka akachukua uamuzi mgumu wa kumbadilisha na kumchezesha kwenye nafasi ya winga.
“Mimi ndiye niliyembadilisha Okrah kutoka kiungo mshambuliaji wa kati akicheza namba 10 na kumchezesha namba 11 akiwa kama winga.
“Nilimbadilisha kutokana na umahiri wake wakutumia vema mguu wa kushoto na anatimiza majukumu yake vizuri.
“Mabadiliko hayo yalitokana na ubora alioonesha mazoezini, tangu nimeanza kumtumia ameonekana kutumika vizuri tangu nilipompa nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza,” amesema.
Kikosi cha Simba kwa sasa kinaendelea na mazoezi kwa ajili ya mechi zao za Novemba na mchezo ujao ni dhidi ya Singida Big Stars.
SOMA NA HII WAKATI SIMBA WAKICHEZA LEO...PABLO ASHINDWA KUJIZUIA..AANIKA YOTE YANAYOENDELEA NDANI...