Home Habari za michezo KUELEKEA MECHI NA WAARABU….YANGA WASOPOZINGATIA HAYA WALA WASIJISUMBE…

KUELEKEA MECHI NA WAARABU….YANGA WASOPOZINGATIA HAYA WALA WASIJISUMBE…

Licha ya matumaini makubwa waliyokuwa nayo mashabiki na wapenzi wa Yanga, mambo yalienda kombo baada ya timu hiyo kulazimishwa suluhu nyumbani ikiwa ni mwendelezo wa mzimu wa kutokuwa sawa katika michuano ya Afrika kila inapotia mguu.

Yanga ikicheza nyumbani ililazimishwa suluhu na Club Africain ya Tunisia katika mchezo wa kwanza wa hatua ya mtoano (play-off) wa Kombe la Shirikisho Afrika.

Matokeo hayo yanakuja ikiwa timu hiyo ikitoka kutupwa nje ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kufungwa na Al Hilal ya Sudan kwa jumla ya mabao 2-1, ikilazimishwa sare ya 1-1 na kulala 1-0 ugenini na kuangukia hatua hiyo ya play-off ya shirikisho ambapo imeanza kwa suluhu.

UCHOVU ULIONEKANA

Katika mechi ya juzi, Yanga haikuwa na mzuka kama ilivyokuwa dhidi ya Al Hilal ikiwa nyumbani, kwani nyota wake walionekana kuwa wachovu pengine kutokana na fatiki ya kucheza mechi mfululizo za Ligi Kuu Bara.

Yanga imecheza mechi nne ndani ya muda wa siku 10, hii ni ratiba ngumu kuanzia Oktoba 23 ilipocheza dhidi ya Simba kisha siku tatu baadaye ikacheza dhidi ya KMC, kabla ya kusafiri tena hadi Mwanza kucheza na Geita Gold na kugeuza kuwahi mchezo huo wa juzi.

Hii ni ratiba ngumu ambayo ni vigumu kwa klabu yoyote kucheza kwa ubora na kupata matokeo bora katika mlundikano wa namna hiyo.

Yanga ilionekana kuathirika na uchovu mapema tu baada ya wapinzani wao kucheza soka la kujihami na kujilinda ambapo walikosa ubora wa kuufungua ukuta wao na kupata mabao kama ambavyo walikuwa wanatamani.

Ukiangalia winga Bernard Morrison, Stephane Aziz KI, Feisal Salum, Fiston Mayele walijieleza wazi jinsi ya mchoko ulivyowaathiri katika mchezo huo wa juzi, hawakuwa na utulivuy kichwani wa ubunifu wa kupenya ngome ya Club Africain.

TUISILIA BADO SANA

Winga Tuisila Kisinda alistahili kutolewa mapema katika mchezo huo ni bahati kwake kumaliza dakika 45 za kwanza kutokana na kutokuwa na jipya. Mtaji wake mkubwa ulikuwa ni mbio na hakukuwa na nafasi ya kufanikisha hilo kutokana na wapinzani wao hawakuwa na akili ya kushambulia kabisa na mabeki wao wa pembeni kuvuka hata nusu ya uwanja.

Kisinda hakuwa na mbinu nyingine za kupenya na hata alipopata nafasi ya kutaka kukimbia mbio zake alijikuta ameshaumaliza uwanja na kuonekana wa kawaida.

WATUNISIA IMEZUGA

Club Africain ilitumia mfumo wa 4-5-1, hawakuwa na ubora kabisa wa kutaka kushambulia walicheza nyuma muda mwingi wa mchezo, walipoteza muda wanavyotaka na bahati njema kwao hawakuwa na wakati mgumu kutoka kwa Mwamuzi Celso Alvacao kutoka Msumbiji ambaye alionekana kuwalea badala ya kuwaadhibu.

Kifupi ni kama Club Africain ilikuja kuzuga Dar es Salaam ikiwa imeweka silaha zao kwa mechi ya marudiano wiki ijayo pale Tunis, Tunisia.

NABI PRESHA TUPU

Katika mazingira magumu kama ambayo Yanga inapitia sasa, hasa katika kukosa matokeo bora lazima mtu wa kwanza kumulikwa ni kocha mkuu wa timu hiyo, Nasreddine Nabi kwa kuwa Yanga inategemea ubunifu wake katika kutengeneza mbinu za kupenya katika mazingira kama hayo.

Hata hivyo, ni kama kocha alivurugwa na kile kilichotokea kwa wapinzani wao waliokuwa wakijiangusha na kupaki basi muda mrefu nakumtibulia mipango, huku akishindwa kufanya maamuzi ya haraka kumlainishia kazi na kujiweka kwenye presha kubwa kutoka kwa mashabiki wa klabu hiyo.

NAFASI BAO IPO

Ukiacha kupoteza dhidi ya Al Hilal lakini rekodi inaonyesha Yanga inacheza vizuri ugenini na hata kama itapoteza huwa inabadilika zaidi kuliko inavyocheza nyumbani.

Suluhu hiyo ni matokeo bora kwa Yanga kwani kama Waarabu hao watafunguka ugenini na Yanga kupata nafasi inaweza kupata bao kwa kuwa sio timu ngumu sana itategemea na mbinu za kocha wao, Nabi katika mchezo huo wa ugenini.

MSIKIE NABI

Kocha Nabi mara baada ya mchezo huo aliutaja uchovu kuwaathiri akisema ilikuwa vigumu kwao kupata matokeo katika mazingira magumu kama hayo huku pia akiwataja Club Africain kuwa haikucheza kama ambavyo huwa inacheza ugenini.

“Nilisema wiki nzima hii tuko katika mazingira magumu katika mechi zetu kutokana na ratiba hii ambayo tumeipitia ndani ya siku 11. Hii ni ratiba ambayo nimeiona kwa Yanga pekee tangu nimefika hapa, nawashukuru viongozi wangu walipambana kuomba lakini imekuwa vigumu kukubaliwa, hatukuchukuliwa kama tunaliwakilisha taifa,”alisema Nabi.

“Nawajua Club Africain hii ni mechi ambayo haikucheza kabisa ilikuwa wengi nyuma ya mpira walichotaka ni kuzuia tu kwa uchovu wetu kuna ubora wa ubunifu tuliukosa, tutakwenda kupambana nao ugenini.

“Mimi sio kocha wa kukata tamaa wala wa mbinu za kujilinda tutakwenda kushambulia hukohuko ugenini tukiwa pia na nidhamu ya ulinzi, hatuna cha kupoteza, tutapata siku chache za kupumzika na kujiandaa.”

Yanga sasa inalazimikia kupambana ipate japo sare ya aina yoyote ya mabao au ishinde ili kutinga makundi ya michuano hiyo itakayokuwa mara ya tatu kwao baada ya 2016 na 2018, huku ikiwa ilitinga makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika mara ya mwisho 1998.

SOMA NA HII  HUU NDIO UMAFIA WALIOUFANYA YANGA DHIDI YA SIMBA KWA MUSONDA...PICHA LILIANZIA HAPA..