HATIMAYE uongozi wa Yanga umewaacha kwenye mataa wapinzani wao Club Africain baada ya kufanikiwa kugundua mitego mizito, jambo lililowafanya kwenda kuweka kambi nje ya Jiji la Sousse nchini Tunisia.
Yanga imekwea pipa kuelekea nchini Tunisia kwa ajili ya mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho dhidi ya timu hiyo, msafara ambao umejumuisha watu 41, kati yao wachezaji 22, viongozi wa benchi la ufundi 10 na viongozi wengine nje ya benchi ni tisa.
Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe amesema ameweka wazi kuwa, wanaenda kupambana kupata ushindi ugenini wakiwa tayari wana taarifa sahihi juu ya mazingira ya huko, ambapo kutokana na kujiridhisha kwa taarifa hizo kikosi chao kitaweka kambi ya siku mbili katika mji wa Sousse, uliopo umbali wa saa mbili na watakapochezea.
“Tunatarajia kuanza safari mapema leo (jana) tukipitia Dubai ambapo tutalala na Novemba 5, 2022 tutaendelea na safari kwenda nchini Tunisia na kuwasili kwenye uwanja wa ndege wa Carthage, mjini Tunisia.
“Kutokana na kujiridhisha na taarifa za watu wetu waliotangulia huko baada ya kuwasili Tunisia, hatutaweka kambi kwenye mji tutakaochezea kwa maana ya ulipo Uwanja wa Hammedi Agrebi Olympic.
“Ila tutaweka nje yam ji huo na Novemba 7, 2022 jioni ndiyo msafara wetu utarejea kupumzika kabla kesho yake Kwenda huko, kwa ajili ya mazoezi ya mwisho kabla ya mchezo wetu na hii ni kutokana na kutafuta utulivu zaidi wa wachezaji baada ya kugundua baadhi ya mambo muhimu nchini humo,” alisema Kamwe.