ALIYEKUWA mshambuliaji wa Yanga, Mkenya Boniface Ambani, amewataka viongozi wa klabu yake hiyo ya zamani kuweka mikakati kwenye mashindano ya kimataifa na kuacha utamaduni wa kusajili kwa ajili ya kuifunga Simba tu kwenye mashindano ya ndani.
Ambani ameyasema hayo baada ya kikosi hicho kushindwa kutinga hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika na kujikuta kikiangukia kucheza mechi ya mchujo kuwania kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho.
Yanga waliianza michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika wakiibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Zalan fc ya Sudan Kusini kabla ya kushinda tena mabao 5-0 mchezo wa marudiano mechi zote zikipigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Baada ya kuvuka hatua hiyo ya awali, raundi ya kwanza ilikutana na wakongwe wa michuano hiyo, Al Hilal ya Sudan, ambapo mchezo wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa ililazimishwa sare ya bao 1-1 kabla ya kufungwa 1-0 ugenini na kuangukia Kombe la Shirikisho ambapo leo inakibarua kigumu ugenini dhidi ya Club Africain ya Tunisia baada ya mechi ya awali hapa nchini kulazimishwa sare tasa.
Ambani, alisema uongozi wa klabu hiyo unatakiwa kujipanga vizuri mwanzo wa msimu ili kufanya vizuri kimataifa, hivyo unapaswa kufanya usajili wa wachezaji wenye uwezo mkubwa kwa ajili ya michuano hiyo.
Alisema Yanga imekuwa ikishindwa kufanya vizuri kwa sababu ya kutokuwa na mipango ya kuandaa timu ikiwamo kusajili wachezaji ambao wataenda kupambania timu kimataifa.
“Viongozi wa Yanga ni shida hasa upande wa usajili wa wachezaji kwa ajili ya mechi za kimataifa na mipango yao ni kuangalia kuwafunga Simba na kushinda ligi ya ndani tu.
“Tofauti na Simba wametoka huko baada ya kufanya vizuri misimu minne nyumbani na kuweka mipango ya kwa ajili ya kufanya vizuri kimataifa, hivyo [kumulika]usajili na hata mipango yao ya mwanzo wa msimu,” alisema Ambani.
Alisema uongozi unatakiwa kufanya usajli mkubwa ukiachilia wale 11 ambao wanacheza kikosi cha kwanza lakini kuna wanaokaa benchi kunatakiwa kuwapo na watu wenye uwezo wa kucheza hizo mechi.
“Yanga wana kila kitu ikiwamo fedha ambazo wanaweza kusajli mchezaji yeyote, kwa mfano ukiangalia safu ya ushambuliaji, Fiston Mayele ni mshambuliaji mzuri, lakini hana mwenzake wa kumsaidia.
Panatakiwa kusajiliwa mshambuliaji mwingine mwenye uwezo kama wa Mayele au zaidi ya hapo. Naamini wakifanya hivyo na maeneo mengine wanaweza kufika mbali. Walisajili kwa ajili ya kuwafunga Simba tu,” alisema Ambani.