Afisa Habari wa Klabu ya Young Africans Ally Kamwe amefichua siri ya ushindi uliowavusha hadi Hatua ya Makundi Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya Club Africain ya Tunisia.
Young Africans jana Jumatano (Novemba 09) iliibuka na ushindi wa 1-0 ugenini mjini Tunis, Tunisia kwenye mchezo wa Mchujo Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
Kamwe ambaye ni sehemu ya viongozi waliosafiri na timu hadi nchini Tunisia amesema kilichofanyika kabla ya mchezo huo wa Mkondo wa Pili, ni hamasa kwa wachezaji ambao walibeba mzigo wa kuivusha Young Africans.
Amesema wanatambua Mashabiki na Wanachama wengi walikuwa wameshakata tamaa na timu yao, lakini mkakati ulioandaliwa na Viongozi kwa wachezaji ulisaidia kupata matokeo yaliyoshtua.
“Tunamshukuru sana Mungu. Mengine yote nitaongea, lakini kubwa tunamshukuru Mungu.Mashabiki wetu walishakata tamaa na timu yao kuelekea katika pambano hili, lakini kama viongozi tulikaa pamoja na wachezaji na kuzungumza nao”
“Ambacho watu wengi hawakijui kulikuwa na tukio la shabiki wa Club Africain kufa na ikatajwa waliomuua ni Polisi, hivyo mashabiki wao walikuja kiwanjani wakiwa na mzuka wa maana.Mashabiki walibishana na Polisi bila woga. Sijawahi kuona nilichokiona. Lakini kama timu tulishikana pamoja na kufanya kilichotuleta hapa Tunisia.”
“Ushindi huu unakwenda kwa mashabiki wetu. Shabiki anapaswa kufahamu kuwa kuna nyakati nzuri na mbaya katika timu. Si timu nyingi zinaweza kushinda nyumbani kwa Mwarabu,” amesema Ally Kamwe.
Young Africans inaungana na klabu nyingine 15 zilizotinga Hatua ya Makundi Kombe la Shirikisho Barani Afrika msimu huu 2022/23 ambazo ni ASEC Mimosas (Ivory Coast), Diables Noirs (Congo Brazzavile), Eloi Lupopo (DR Congo) Future FC (Misri), Al Akhdar (Libya) AS Real(Mali), Marumo Gallants( Afrika Kusini) ASKO (Togo)Pyramids (Misri), USMA(Algeria), TP Mazembe (DR Congo), DC Motemba Pembe Congo), AS FAR(Morocco), Rivers United (Nigeria) na Monastir (Tunisia).