Home Habari za michezo MEXIME: NIMEONA UDHAIFU WA YANGA…WATU WANATAKA USHINDI TU..

MEXIME: NIMEONA UDHAIFU WA YANGA…WATU WANATAKA USHINDI TU..

Kocha wa Kagera Sugar, Mecky Maxime ameipongeza Yanga kwa ushindi ilioupata ugenini nchini Tunisia dhidi ya Club Africain na kucheza mpira mkubwa huku akitamba kuwa hilo haliwatishi kwani wamejiandaa vya kutosha kuchukua pointi tatu kesho dhidi mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu.

Kagera Sugar itaikaribisha Yanga kesho katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza mchezo huo ukipigwa kuanzia saa 10 jioni huku mashabiki wakitakiwa kulipa Sh 5,000 (mzunguko), Sh 10,000 (VIP B na C) na Sh 20,000 kwa jukwaa kuu.

Maxime ambaye ni mchezo wake wa pili tangu ajiunge na Kagera Sugar amesema aliwatazama Yanga wakipindua meza uarabuni hivyo ameona mapungufu na ubora wao ambao ameufanyia kazi na anaamini utampa matokeo mazuri kesho.

“Tunawaheshimu Yanga tunajua wametoka Tunisia wako vizuri lakini tunataka pointi tatu. Nimeanza kuingia philosophy na utamaduni wangu taratibu nafikiri tunakwenda vizuri tumepata wiki moja ya kujiandaa na mambo yanakwenda vizuri,”

“Nakwenda kucheza na Yanga nimeangalia ubora na udhaifu pamoja na nguvu yetu iko wapi kwahiyo vyote hivyo tumevifanyia kazi kwenye uwanja wa mazoezi tunategemea vitatulipa. Mimi ni mwalimu wa mpira nineshakubali kazi watu wanataka ushindi, hivyo nahitaji kutimiza hilo kama ambavyo walionileta wanategemea,” amesema Maxime.

Kocha huyo amewaomba mashabiki kuja kwa wingi kwani mechi itakuwa nzuri kutokana na kilichoonyeshwa na Yanga nchini Tunisia huku Kagera Sugar iliyo chini yake ikianza kuimarika hivyo mtanange huo utakuwa na burudani kubwa.

Nahodha wa Kagera Sugar, David Luhende amesema wamejiandaa kikamilifu na wapo tayari kupata matokeo kwani wamefanya mazoezi yao vizuri na wamekalishana chini na kuweka mipango kabambe itakayowapa alama tatu dhidi ya Yanga.

“Mwalimu ameshatimiza wajibu wake kwa kutupa maelekezo na sisi kesho ndiyo tunakwenda kuthibitisha kile tulichokifanyia kazi hivyo tuna ujasiri mkubwa kuwa kesho tutapata ushindi,” amesema Luhende.

SOMA NA HII  WAKATI VYUMA VIPYA VIKITAJWA KUTUA ...GAMONDI AWAPIGA MKWARA MASTAA YANGA...