KIKOSI cha Yanga baada ya kutua nchini, wachezaji na viongozi wao wakitembea kwa kuvimba baada ya ushindi na kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika na wamesema kwamba “sasa tuna mzuka aje yeyote makundi.”
Kikosi hicho kilipotua kilikaa muda mchache Dar es Salaam kabla ya kuunganisha ndege kwenda jijini Mwanza ambako leo Jumapili watacheza mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Kagera Sugar ndani ya CCM Kirumba.
Bao la Stephane Aziz Ki la dakika ya 79 lilitosha kuipa Yanga ushindi wa bao 1-0, ugenini Tunis Alhamisi ya wiki hii na kutinga hatua ya makundi kwa mara ya tatu katika miaka sita baada ya kufanya hivyo pia 2016 na 2018. Jambo lililowaongezea mzuka Wananchi hao na sasa wanatamba wapo tayari kukabiliana na vigogo wengine wa Afrika watakaopangwa nao kwenye makundi bila woga wowote na wako fiti ndani na nje ya Uwanja.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Rodgers Gumbo alisema akili yao sasa ni kuhakikisha hadhi ya timu hiyo inarejea kimataifa kwa kufanya makubwa zaidi kwenye makundi.
“Tunarudi kwenye Ligi tukiwa na morali mpya, tunataka kuendelea kutetea mataji yetu ya msimu uliopita na kikosi chetu kimethibitisha afya yake baada ya soka ambalo tumelipiga kule Tunisia.
“Tunasubiri ratiba ya CAF kujua makundi yatakuwaje, tunaziheshimu timu zote zilizokata tiketi ya kucheza makundi na utaona zilistahili lakini Yanga hatuna cha kuhofia, tukijua ratiba tutajipanga kukabiliana na mpinzani yeyote atakayekuja mbele yetu.”
Gumbo aliongeza kuwa bado hawajajua kama watafanya usajili wa aina gani katika dirisha dogo na kwamba hilo wanawaachia makocha ingawa wanaamini bado wachezaji wao waliopo wana nguvu ya kuipigania timu yao.
“Ukiangalia kuna wachezaji ambao walikuwa hawatumiki lakini wameanza kupewa nafasi na wanaonyesha ubora wao, nadhani watu walimuona Baca (Ibrahim Abdallah) alivyocheza mechi za ligi lakini pia kuna Sure Boy hakucheza mechi ya kwanza na Club Africain hapa ila kule akapewa nafasi akaushangaza ulimwengu.
“Timu tunayo, tunawaachia makocha waendelee kuwatumia vijana tulionao kwasasa isipokuwa tutasubiri ratiba ya mechi zinazokuja na kuwasikiliza makocha wanahitaji kipi tukiona kuna ulazima Yanga itaingia sokoni.”
Katika mapokezi Dar jana, Nabi hakuwa na maneno mengi; “Asanteni. Tumesahau matokeo sasa akili ipo kwa Kagera Sugar. Kile kilichoonyeshwa tunatarajia kukiendeleza kwenye mchezo ujao.” alisema.
Rais wa Yanga, Hersi Said alisema; “Tunajiandaa kwaajili ya mapambano zaidi baada ya kupata nafasi ambayo tumeipambania kwa hali na mali kwa zaidi ya miaka miwili, sasa akili zote ziko kwenye mchezo wa Jumapili tunahitaji matokeo.”
KUKUTANA NA HAWA
Katika droo hiyo, timu 16 zilizofuzu makundi zitapangwa kwenye makundi manne kutokana na ubora na pointi zao kwa miaka mitano iliyopita.
‘Poti’ ya kwanza itakuwa na timu nne zilizofanya vizuri zaidi kwa miaka ya hivi karibuni kwenye michuano ya CAF ambazo ni TP Mazembe (DR Congo), Pyramids (Misri), Asec Mimosas (Ivory Coast) na USM Alger (Algeria).
Katika timu hizo nne, Yanga itakutana na moja tu kwenye hatua ya makundi na nyingine tatu zitagawanywa kwenye makundi mengine.
Yanga iko kwenye ‘Poti’ ya pili pamoja na Motema Pembe ya DR Congo lakini timu hizo mbili haziwezi kukutana kwenye kundi moja lakini zitapangwa dhidi ya timu nyingine, moja kutoka poti namba moja ile ya kina TP Mazembe na timu nyingine mbili kutoka kwenye moja kati ya poti ya tatu na poti ya nne.
Kwa maana hiyo Yanga huenda itakutana na kigogo mmoja kati ya Mazembe, Pyramids, Asec na USM Alger na timu nyingine mbili ambazo ni za kawaida kutokana na rekodi zao kutofikia zile za Yanga kimataifa kwa misimu mitano ya hivi karibuni.
Hata hivyo, Yanga haipaswi kubeza timu hizo kwani miongoni mwake ni zile zilizofanya usajili mkubwa msimu huu na zimekuwa zikicheza kwa ubora.
Timu hizo ni Al Akhdar ya Libya iliyoiondosha Azam msimu huu kwa jumla ya mabao 3-2, nyingine ni Rivers United ya Nigeria iliyoitoa Yanga msimu uliopita kwenye mtoano wa Ligi ya Mabingwa Afrika ikishinda nyumbani na ugenini bao 1-0 kwenye kila mchezo.
Wengine ni AS FAR ya Morocco timu aliyotoka Yannick Bangala akitua Jangwani lakini pia msimu uliopita ilikuwa ikinolewa na kocha wa zamani wa Simba, Sven Vandenbroek na kuifanya kumaliza msimu ikiwa kwenye nafasi tano za juu za ligi ya Morocco.
Timu nyingine ni Diables Noirs ya Congo Brazzaville, Saint Eloi Lupopo ya DR Congo ambayo Mussa Mgosi aliwahi kuichezea, Future ya Misri, Real Bamako ya Mali, Marumo Gallants ya Afrika Kusini, ASKO Kara ya Togo na US Monastir ya Tunisia.
REKODI ZAO ZIKOJE
Yanga kwa miaka ya hivi karibuni imeburuza mkia katika hatua ya makundi mara mbili katika Kombe la Shirikisho, mwaka 2018 na 2016, hivyo msimu huu inapaswa kujipanga zaidi kwani itakutana na timu zenye ubora na historia nzuri na michuano hiyo.
TP Mazembe imetwaa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika mara tano na Kombe la Shirikisho mara mbili lakini pia msimu wa 2019/2020 ilifika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na msimu wa 2020/2021 iliishia makundi ya michuano hiyo huku mara ya mwisho kushiriki Shirikisho ilikuwa mwaka 2017 ilipobeba ubingwa.
Timu nyingine itakayoleta ushindani kwa Yanga kama zitapangwa pamoja ni Pyramid ya Misri ambayo imekuwa ikishiriki mara kwa mara michuano hiyo na mafanikio yake makubwa ilikuwa msimu wa 2019/2020 ilipofika fainali na kufa 1-0 mbele ya RS Berkane na msimu huo ilikutana na Yanga kwenye mtoano na kuitoa ikiichapa 3-0 nyumbani na ilivyokuja Bongo mechi ikapelekwa CCM Kirumba Mwanza Yanga ikafa 2-1.
Asec aliyotoka Aziz Ki, ambayo mwaka 2019 iliishia makundi ya Ligi ya Mabingwa, msimu uliopita ilifika makundi ya Shirikisho na kucheza na Simba ikishinda 3-0 nyumbani na kuchapwa 3-1 kwa Mkapa.
IKIFANYA HIVI
Yanga inatakiwa kuboresha kikosi chao kwenye dirisha dogo la usajili ili kupata wachezaji wazuri maeneo iliyokuwa na upungufu kama beki wa kati, kushoto na straika mwingine atakayempa ushindani wa Fiston Mayele.
Viongozi na mashabiki wa Yanga wanatakiwa kuungana na kuona hayo mashindano ni sehemu ya maisha yao.